Patanisho: Jamaa aficha simu, nguo za mwanadada asiyempenda kwa lengo la kumlazimisha ndoa

Apia aliweka wazi hakuwa na hisia zozote za mapenzi kwa Kemboi na akasimulia jamaa huyo alivyolazimisha mambo.

Muhtasari

•Kemboi alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja iliharibika baada ya mkewe kuanza madharau na kukataa kuishi kwao.

•Apia alipopigiwa simu alibainisha wazi kwamba hana chochote cha kuzungumza na jamaa huyo.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Dan Kemboi ,25, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Apia Namukoye ,22, ambaye alikosana naye mwezi uliopita.

Kemboi alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja iliharibika baada ya mkewe kuanza madharau na kukataa kuishi kwao.

"Tulikuwa tunaishi naye vizuri vile tulikuwa nyumbani. Nikirudi jioni naskia mara wamegombana. Nikiuliza dada zangu wanasema bibi yangu ako na madharau. Niliamua kuenda kujenga mahali pengine niishi vizuri na bibi yangu. Nikakosa pesa ya kujenga.

Nilisema nikatafute kitu ndio nipate pesa ya kujenga. Akasema hawezi kuachwa nyumbani lazima tuende naye. Tulienda naye nikamtafutia kazi ya boma. Baada ya mwezi mmoja, akaanza kuniongelesha vibaya hadi akaniblock.Hajaniambia chochote na ameniblock. Sijaona mahali nimemkosea pia," Kemboi alisimulia.

Apia alipopigiwa simu alibainisha wazi kwamba hana chochote cha kuzungumza na jamaa huyo.

Aliweka wazi kwamba hakuwa na hisia zozote za mapenzi kwake na akadai kuwa alilazimishwa.

"Sasa tuongee nini ingine na yeye. Tulikosana na yeye kabisa. Huyo kijana sikuwa eti nampenda. Tulikuja huku mwaka jana. Tulikuwa tu marafiki. Nikamwambia anitafutie kazi. Kufika kazi akachukua simu yangu akaficha, akachukua nguo zangu akaficha. Mimi sikuwa na akili ya kuoleka, nilikuwa nataka kuenda shule. Mimi nataka niende kozi kwanza nimalize ndio nifikirie mambo ya kuoleka," Apia alisema.

Aliongeza, "Vile alificha nguo zangu, akasema tuende nyumbani. Tukakaa miezi sita. Na hata hiyo miezi sita hatukukaa vizuri. Alikuwa anaenda anarudi usiku na hakuna kitu alikuwa analeta nyumbani. Mimi sitaki tena. Mimi nashughulika mambo ya shule."

Kemboi hata hivyo alisisitiza kuwa mwanadada huyo alikuwa amekubali washiriki mahusiano na akadai kwamba Apia amemgeuka.

Wawili hao hawakuweza kupatanishwa kwani Apia tayari aliweka msimamo wake wazi na simu zao zilikuwa na matatizo.

Je, maoni yako ni yepi kuhusu Patanisho ya leo?