Patanisho: Jinsi mwanadada alivyogundua mumewe ana mahusiano na jirani aliyeolewa

"Nilithibitisha. Ilikuwa tu jirani wake kwa ploti, mama mwingine hapo. Ni bibi ya mtu," Vivian alisema.

Muhtasari

•Vivian alipopigiwa simu alithibitisha kwamba alibainisha mpenziwe alikuwa na mahusiano na mwanamke jirani wake.

•Vivian hata hivyo alisikika kushikilia msimamo wake na kubainisha kwamba hawezi kurudiana naye.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Collins Ochieng ,28, kutoka Kisumu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Vivian Obuong ,25, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.

Collins alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika Agosti mwaka huu kufuatia fitina za majirani katika ploti.

Alidai kwamba mkewe alimshutumu kwa kuwa na mwanamke mwingine, madai ambayo alitupilia mbali.

"Tulikuwa na mke wangu miaka miwili. Shida ilitokea kwa ploti wakati aliskia maneno ingine eti mara niko na mwanamke ama niko mahali fulani. Kuna mtu alikuwa anaongea naye kwa hii ploti. Alikasirika akaacha kuniongelesha. Sasa hivi niko Nairobi, yeye ako shule Kisumu," Collins alisema.

"Mimi sina mwanamke mwingine, ata sasa hivi sina. Hapa kwa ploti, unajua watoto wanaweza kuingia kwake wakitazama filamu. Kuna mtoto alichukua simu akaenda nayo kwa nyumba yao. Akaenda akapiga picha. Simu yangu ilikuwa na email, picha zikipigwa zinaenda kwa simu ambayo nilimpatia.  Yeye aliziona akasema maneno mengine," aliongeza.

Vivian alipopigiwa simu alithibitisha kwamba alibainisha mpenziwe alikuwa na mahusiano na mwanamke jirani wake.

"Nilithibitisha. Ilikuwa tu jirani wake, mama mwingine hapo. Ni bibi ya mtu. Kuna simu yake nilikuwa nayo na akaunti yake ndiyo nilikuwa natumia. Sasa vitu alikuwa anafanya nilikuwa naona. Akipiga picha hadi akichukua video . Alikuwa anachukua hadi video mpaka huyo mama akiwa amelala kwa kitanda. Alikuwa anapiga picha hadi kwa nyumba ya huyo mama. Alikuwa anaenda nyumba ya huyo mama anakula na kulala.  Nikimuuliza anakataa," alisema.

Collins alijitetea akisema, "Ni mtoto alikuwa anafanya hizo vitu. Alipiga video akionyeshana hiyo nyumba.Ni ile tu hali unaweza kutembelea mtu. Haikuwa usiku sana. Sikuwa nimemtembelea. Tuliongea na Vivian nikakubali ilifanyika. Sikuwa pekee yangu, nilikuwa na vijana wengine. Hao vijana waliondoka wakaniacha."

Alipopewa fursa ya kuzungumza na Vivian, alimwambia, "Vivian mimi nakuomba msamaha kwa kile ambacho kilitokea. Kweli nishapatikana, mimi naomba msamaha tuendelee pamoja."

Vivian hata hivyo alisikika kushikilia msimamo wake na kubainisha kwamba hawezi kurudiana naye.

"Mimi nilikusamehe. Hakuna vile tunaweza kurudiana. Yangu na wewe iliisha hivyo, sitaki stress," alisema na kukata simu.

Collins alithibitisha kwamba tayari amehama ploti ambayo alikuwa anakaa.

Alimwambia mpenziwe, "Mimi bado nampenda. Kama anaweza kufungua roho turudiane ni sawa."

Je, ushauri ama maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?