Patanisho: Baba ajawa uchungu baada ya mtoto aliyemlea kumwambia yeye si baba yake

Bw Oketch alisema licha ya kutomtunga mimba ya mamake Victor, mama yake alimshinikiza amuoe.

Muhtasari

•Victor alisema uhusiano na mlezi huyo wake ulisambaratika mwaka wa 2016 wakati ambapo alimkana kama babake.

•Bw Oketch alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba Victor sio mtoto wake wa kuzaa bali alikuja na mamake wakati alipomuoa.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Victor Odhiambo kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake mlezi Augustine Oketch ambaye alikosana naye takriban miaka saba iliyopita baada ya kumtumia ujumbe wa matusi.

Victor alisema uhusiano na mlezi huyo wake ulisambaratika mwaka wa 2016 wakati ambapo alimkana kama babake.

"Kuna vile walikosana na mama yangu alafu akaenda. Tukabaki na baba. Kazi niliyokuwa nikifanya pale nilikuwa naona kama ananitesa. Tulikuwa tunafanya kazi nyingi naona kama ni ngumu. Tulikuwa tunashinda kwa shamba. Hata hakuwa ananinunulia nguo, nilihisi uchungu," Victor alisimulia.

Aliendelea, "Siku moja nilimtumia ujumbe nikamwambia vile ananifanyia sioni kama yeye ni babangu." 

Victor alifichua kuwa mamake alitengana na baba yake na kutoroka akimuacha yeye na ndugu zake wengine.

Alikiri kuwa kuna watu ambao walikuwa wakimwambia kwamba Bw Oketch sio baba yake mzazi.

"Huwa tunaongea na mama. Huwa namtembelea hata," alisema.

Bw Oketch alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba Victor sio mtoto wake wa kuzaa bali alikuja na mamake wakati alipomuoa.

"Huyo Victor, nikiwa kidato cha pili nikawa rafiki na mama yake, alikuwa darasa la nane. Baada ya muda kidogo nikaona mamake na mimba. Nikamuuliza mamake ametoa mimba wapi na hatujakutana kimapenzi," alisimulia.

Bw Oketch alisema licha ya  kutomtunga mimba ya mamake Victor, mama yake alimshinikiza amuoe ili baadaye aweze kuchukua nafasi ya kaka yake ambaye hakuwa na watoto.

" Wakati nilimaliza kidato cha nne, kakangu akafa. Mama Victor alikuja na mtoto mdogo mchanga anayenyonya. Tukakaa na yeye. Mama Victor aliniacha na watoto nikaoa mwanamke mwingine. Bibi mdogo alisema lazima nimpeleke shule hata kama hajapita kidato cha nne, Victor alikataa kuenda" alisema.

Bw Oketch alisema ni wakati huo ambapo Victor alimtumia ujumbe wa matusi kisha akatoweka kabisa asionekane nyumbani.

"Nilitambua huyo mtoto kama wangu kutoka kitambo. Kibiolojia nilijua sio wangu. Lakini sikuwahi kumwambia," alisema.

Victor alimuomba mlezi huyo wake msamaha na kumwarifu kwamba alichukua hatua mbaya kutokana na hasira.

Bw Oketch alikubali kumsamehe Victor na hata akamruhusu ajenge nyumba katika shamba lake.

Je, una ushauri upi kwa Victor?