Patanisho: Jamaa afungwa na baba yake mchungaji baada ya kutorokea Nairobi

Wycliffe alisisitiza kuwa hakuiba wala kutumia pesa za babake vibaya ila alivamiwa na wezi.

Muhtasari

•Wycliffe alisema alikosana na babake baada ya kuvamiwa na majambazi ambao waliiba kipato cha biashara ya familia pamoja na simu ambazo alikuwa amebeba.

•Bw Wycliffe alimwagiza mwanawe kutuma pesa za sukari kama ishara ya shukrani kwa msamaha.

Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Wycliffe Oduor alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake Bw Emmanuel ambaye walikosana naye kufuatia ugomvi wa pesa.

Wycliffe alisema husiano wake na mzazi huyo wake ulianza kuwa mbaya mapema mwaka huu baada ya kuvamiwa na majambazi na kuibiwa kipato cha biashara ya familia pamoja na simu ambazo alikuwa amebeba.

"Nilikuwa natoka kazi jioni nikavamiwa na wezi wakaninyang'anya pesa za mzee. Kufika kwa nyumba kumuelezea akakataa kuamini. Asubuhi ilipofika nilienda kuripoti kwa polisi lakini bado hakuamini," alisimulia.

Alieleza kuwa juhudi za kuzungumza na babake ili kutafuta suluhu bado hazijaweza kufua dafu.

"Watu wa kanisa walijaribu kuzungumza naye lakini bado hakuamini. Nimejaribu kumuelezea, hadi mama alijaribu kumuelezea lakini akasema tunashirikiana naye kumuibia," alisema.

Wycliffe alifichua kuwa pesa zilizoibiwa ni shilingi 30, 000 ambazo zilikuwa kipato cha biashara ya Mpesa.

"Tulizungumza naye wakati wa matanga ya shangazi tu," alisema.

Bw Emmanuel alipopigiwa simu Wycliffe alichukua fursa kujitetea na kumuomba msamaha kwa yote ambayo yalitokea.

Wycliffe alisisitiza kuwa hakuiba wala kutumia pesa za mzazi huyo wake vibaya na badala yake alivamiwa na wezi.

"Naomba uweze kunisamehe na unifungue maana najaribu kila mbinu lakini sioni nikifaulu,"  alimwambia babake.

Bw Wycliffe alimjibu, "Wewe ni mtoto wangu na siwezi kukutupa. Mzazi ni mzazi. Mimi nimekusamehe"

Mhubiri huyo aliweka wazi kuwa alikasirika baada ya mwanawe kutoroka nyumbani na kuacha biashara ambayo alikuwa amemwekea.

"Nilikuwa nimfungulia kazi akafunga mlango na akaenda Nairobi. Aliacha kila kitu kwa nyumba ya biashara. Mimi kama mzazi nimeshatumia pesa nyingi kwake. Alafu analeta mzaha, akaacha kazi na kuenda Nairobi," alisema.

"Kama ameomba msamaha nimemsamehe,"

Wycliffe alijitetea kwa kusema kuwa wakati alipogura nyumbani alikuwa akihangaika ndiposa akafanya maamuzi mabaya.

"Nakupenda kama baba yangu na nashukuru sana maana umenisamehe," alimwambia babake.

Bw Wycliffe alimwagiza mwanawe kutuma pesa za sukari kama ishara ya shukrani kwa msamaha.

"Mtoto ni wangu na nilikuwa najua nitawekeza kwake maana wale ambao wamemtangulia hawajafanikiwa. Atulie mahali nilimweka kwa sababu baraka zake ziko pale," alisema.