Patanisho: Jamaa aleta mpango wa kando nyumbani, mkewe ampikia ugali na chai bila kujua wanachumbiana

"Tayari umeoa bibi kama sita. Alikuwa unaleta huyu,kesho analeta mwingine. Aliwabadilisha kama nguo," Lydia alilalamika.

Muhtasari

•Wanyonyi alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 9 na kumwachia watoto wawili wadogo baada ya kumpata na mpango wa kando.

•Wanyonyi alisema masaibu yalianza kwenye boma yake baada ya mke wake mpya kujifungua mtoto wao pamoja.

•Lydia alieleza kuwa mzazi huyo mwenzake alimwonyesha madharau makubwa mbele ya mpenzi wake na baba yake.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Evans Wanyonyi ,33, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mkewe Lydia Nafuna ,26, ambaye alikosana naye 2019.

Wanyonyi alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 9 na kumwachia watoto wawili wadogo baada ya kumpata na mpango wa kando.

"Wakati tuliachana na yeye nilikuwa na mpango wa kando. Wakati alipojua, nilijaribu kumweleza akasema hawezi kuvumilia. Tulikuwa na mzozo ambao ulifanya nikawa na mpango wa kando," Wanyonyi alisimulia.

Wanyonyi alieleza kwamba aliamua kutafuta mpango wa kando baada ya kumshuku Lydia kuwa na mwanaume mwingine.

"Nilikuwa nafanya kazi ya bodaboda. Niliacha pikipiki kwa mama yangu nikateremka nyumbani nikapata anaongea na mwanaume kwa simu. Mwanaume alimuuliza kama bado ako nyumbani akasema ako kwa shangazi," alisema.

Aliongeza, "Ilifika mahali nikamwambia kama ameamua hivo acha ata mimi nijipanga. Aliondoka akaniachia mtoto wa miaka miwili na mwingine wa miaka minne. Nilijaribu kumfuatilia kwa simu akasema hawezi kurudi."

Wanyonyi alikiri kwamba baada ya kukaa pweke kwa muda alitafuta mke mwingine ambaye alizaa naye mtoto mmoja.

Hata hivyo, alisema masaibu yalianza kwenye boma yake baada ya mke wake mpya kujifungua mtoto wake.

"Ilifika mahali ikabidi nimetafuta mwenzangu ambaye alikubali kukaa na watoto. Ilifika mahali akajifungua wake. Tuko na mtoto mmoja na yeye... Kusema kweli, watoto wangu wanaumia. Imefika mahali akajifungua, watoto wangu wanaumia. Ningetaka tuzungumze suala la watoto. Alikataa kurudiana na mimi," Wanyonyi alisema

Lydia alipopigiwa simu alisikika kushangaa kwa nini Wanyonyi alikuwa akimtafuta ilhali ako na mke mwingine;

Aliibua madai kwamba mume huyo wake wa zamani amekuwa akioa mke mwingine baada ya mwingine.

"Tayari umeoa bibi kama sita. Alikuwa unaleta huyu,kesho analeta mwingine. Aliwabadilisha kama nguo," alisema.

Alimwambia Wanyonyi, "Mara ya mwisho nilikuja kwenu ukasema huyo bibi uko naye ulienda ukaomba kwao, eti mimi uliniokota."

Lydia alieleza kuwa mzazi huyo mwenzake alimwonyesha madharau makubwa mbele ya mpenzi wake na baba yake.

"Siku moja aliniletea mwanamke nikapika ugali na chai tukakula na yeye. Kumbe ni mwanamke wake.. Huyo alienda, akaleta mwingine.. baba yake alisema anapenda mimi. Akasema hataki mimi anataka huyo," alisema.

"Juzi walinipigia simu akasema nataka kuua mke wake na mtoto wao, sijui alimaanisha vipi na mimi siko huko.. Akitaka kunipea watoto ni sawa.  Mimi ndiye nasaidia watoto. Karo ni mimi nalipa. Mimi niko tayari kuchukua watoto."

Wanyonyi  hatimaye alikubali kuwapeleka watoto kwa mamake Lydia, jambo ambalo Lydia alikubaliana nalo.

"Mimi nimekubali kukupatia watoto na sina ubaya na wewe. Ukilemewa mahali unaweza kuniambia," Wanyonyi alisema.

Lydia alimwambia, "Mimi nilikuwa nakupenda lakini ukanifanyia vibaya. Kama umeamua kunipatia watoto nashukuru."