Patanisho: Jamaa amcheza mkewe kwa kuhamisha nguo, TV, redio polepole kabla ya kutoweka kabisa

Wasike aliweka wazi kuwa alimpenda sana mzazi huyo mwenzake ila alicheza na hisia zake.

Muhtasari

•Wasike alisema mumewe aliondoka nyumbani akidai ameenda Narok kwa ajili ya kazi lakini baada ya muda akahama kabisa.

•Wasike alidai kwamba Bw Otieno alichukua redio na TV kwa nyumba akidai kuwa anaenda kuzipeleka kwa fundi.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Nowell Wasike ,42, kutoka Webuye alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Mark Otieno, 50, ambaye alimuacha takriban miaka mitano iliyopita.

Wasike alisema mumewe aliondoka nyumbani akidai ameenda Narok kwa ajili ya kazi lakini baada ya muda akahama kabisa.

"Aliniacha Naivasha na watoto akaenda kazi Narok. Akawa anakuja wiki za kwanza alafu ikafika mahali akawa hakuji. Kwa kuwa miezi kadhaa ilipita bila yeye kuja, majirani wakaanza kuniuliza kuna nini. Nikawadanganya huwa anakuja usiku alafu anaenda kwa sababu niliona aibu kuwaeleza ukweli" alisema.

Wasike alisema kuwa baada ya kushuku mambo hayakuwa sawa alimpigia simu mumewe kujua kinachoendelea. 

"Wakati niligundua ameniacha nilimpigia simu nikitaka kufungiwa nyumba. Akaanza kuwa mkali. Wakati huo niligundua kumbe hata hakuna nguo zake kwa nyumba. Alikuwa anakuja anachukua nguo zake kadhaa anaenda," alisimulia.

 Wasike alidai kwamba Bw Otieno pia alichukua redio na TV kwa nyumba akidai kuwa anaenda kuzipeleka kwa fundi. Alisema kuwa vifaa hivyo vya nyumba havikuwa vimeharibika wakati mumewe alipovichukua. 

"Nimeteseka sana na watoto. Hata mama yangu aliaga, hakuhudhuria mazishi. Alienda mwaka wa 2018.Yeye hajawahi kunipigia hata mara moja. Sasa hivi niko Nairobi," alisema.

Aliongeza, "Nikimuuliza kuhusu watoto anasema niwaweke kwa gari waende. Nashangaa kwani watoto ni mzigo. Yeye huwa na madharau sana!" 

Wasike aliweka wazi kuwa alimpenda sana mzazi huyo mwenzake ila alicheza na hisia zake.

"Nimehangaika na watoto.  Sijawahi kugombana na yeye. Hata hajawahi kulalamika. Yeye ni mtu wa raha nyingi. Kuna wakati tukiwa tumelala angepigiwa simu," alisema.

Juhudi za kumpatanisha Wasike na mumewe hata hivyo hazikufua dafu kwani Bw Otieno alikuwa amezima simu.

Je, ushauri wako kwa Wasike ni upi?