Patanisho: Jamaa amtusi mama mkwewe vibaya baada ya kukataa bintiye aolewe kwa "maskini"

"Tulienda mama yake akatutusi . Enyewe ata mimi nilimtusi kidogo," Wafula alisema.

Muhtasari

•Wafula alisema uhusiano wake na mama mkwe uliharibika mwezi Februari baada ya kukabiliana naye kwa matusi alipokataa ndoa yake na bintiye.

•Mamake Diana aliweka wazi kwamba hana shida na Wafula na kumhakikishia kwamba mkewe anaendelea vizuri.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Jacob Wafula ,23, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama mkwewe Janet Nanjala ,60, ambaye alizozana naye mapema mwaka huu.

Wafula alisema uhusiano wake na mama mkwe uliharibika mwezi Februari baada ya kukabiliana naye kwa matusi alipokataa ndoa yake na bintiye.

"Tulikuwa tumeoana na msichana wake 2022. Ilifika mahali nikataka kumpeleka nyumbani ajue watu wetu kwani tuliishi Nairobi. Kufika akaanza kusema eti huko anaboeka eti hajawahi kukaa mahali kama huko. Nikasema acha turudi Nairobi," Wafula alisimulia.

Aliendelea, "Ikafika Januari 2023 nikamwambia nataka tuende tujue kwao nikamuomba aambie wazazi tunaenda. Alienda kwao na mimi nikaenda nikapanga wazee tukaenda. Kufika huko tukakuta mambo yamebadilika. Kumbe alienda akaambia mamake hawezi kukaa mahali kwa maskini. Wazee walijaribu kumuongelesha lakini hakusikia. Alisema kama ni mtoto tungoje azae alafu tuende tumchukue."

Alisema baada ya kurudi nyumbani alipanga ziara nyingine na ndugu zake ambapo hawakupokelewa vizuri pia.

"Tulienda mama yake akatutusi . Enyewe ata mimi nilimtusi kidogo. Sasa ata msichana wake aliniblacklist hatuwezi kuwasiliana. Tumeongea na mzee wake anasema nipange siku niende," Wafula alisema.

Wafula alisisitiza kwamba ata kama hatarudiana na mkewe ambaye ni mjamzito angependa kuwajibikia mtoto baada ya kuzaliwa.

Mamake Diana alipopigiwa simu mwanzoni alikuwa mkali hadi kukata simu ila akawa mtulivu katika jaribio la pili.

Aliweka wazi kwamba hana shida na Wafula na kumhakikishia kwamba mkewe anaendelea vizuri.

"Mimi sitaki kuongea. Mimi sina shida na yeye. Msichana ako poa, hajajifungua bado. Wafula anakaribishwa nyumbani," alisema.

Wafula alisema atapiga hatua ya kuwasiliana na wakwe zake katika jaribio la kusuluhisha mzozo wao.