Patanisho: Jamaa aomba walevi wachezewe wimbo 'Pombe ina madhara' baada ya ulevi kuvunjwa ndoa yake

"Siku moja nilikunywa pombe ya hasira, nikaingia kwa nyumba nikatusi mke wangu. Keshoye aliamka akaenda," Wanjohi alisema.

Muhtasari

•Wanjohi alisema ndoa yake ya miaka saba ilisambaratika Machi mwaka huu baada ya yeye na mkewe kuvuragana kwa nyumba.

•Njeri alisisitiza kwamba mumewe ameagizwa kupiga hatua ya kuenda nyumbani kwao ili kutatua masuala yao.

Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Wanjohi Kariuki ,32, kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa  na mke wake Edith Njeri ,29, ambaye alikosana naye takriban miezi mitatu iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Wanjohi alisema ndoa yake ya miaka saba ilisambaratika Machi mwaka huu baada ya yeye na mkewe kuvuragana kwa nyumba.

Alisema alikunywa pombe akaenda nyumbani na hasira nyingi na kumtusi mkewe, jambo ambalo lilimkasirisha akaenda.

"Nilikuwa mtu wa kunywa pombe. Siku moja nilikunywa pombe ya hasira, nikaingia kwa nyumba nikatusi mke wangu. Keshoye aliamka akaenda. Saa hii anasema ako Nyeri anasema ako kazi," Wanjohi alisema.

Aliongeza, "Mimi mwenyewe nimeachana na pombe, nimepunguza. Nimeachana nayo kabisa. Niko na wiki kama tatu hivi."

Njeri alipopigiwa simu alikiri kwamba aligura ndoa yake kutokana na tabia ya mumewe ya ulevi na matusi kwa nyumba.

"Ni hiyo tu mambo ya pombe na matusi. Akikunywa kazi yake ni matusi," Njeri alisema.

Wanjohi alijibu, "Mimi nimebadilika, nimeacha hayo mambo. Naomba urudi kwako tuendelee na maisha. Mimi nimeachana na hayo mambo."

Njeri alisisitiza kwamba mumewe ameagizwa kupiga hatua ya kuenda nyumbani kwao ili kutatua masuala yao.

Aidha, aliomba muda wa kuponya moyo wake kabla ya kufanya uamuzi.

"Nilimwambia anipe muda nipone, nilimwambia aje mwezi wa tisa," alisema kisha akakata simu.

Wanjohi alisema, "Nitajipanga mwenyewe. Kwangu nimebadilika na nimeng'ang'ana kabisa kubadilika kwa sababu ningependa ndoa yangu isimame.. Nilianza na muratina lakini saa hii niko Kajiado. Nilianza kitambo lakini imefika mahali nikabadilika."

Pia aliomba kuchezewa ngoma maalum iwaendee walevi wote kama tahadhari.

"Wekea walevi wote ngoma ya Rose Muhando 'Pombe ina madhara' Kama ilifanya ndoa yangu ivunjike, walai nitaacha. 

Mama Jeremy nampenda sana. Kama sio yeye, sioni mambo ingine mbele yake. Afanye uamuzi wa kurudi kwake. Ajue mimi nampenda na namheshimu," alisema Wanjohi.

Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?