Patanisho: Maajabu huku Kelvin akitaka kupatanishwa na jamaa aliyemfumania na mkewe kitandani usiku

Kelvin alidai kwamba mke wa Bruno alikuwa ametorokea kwake usiku baada ya kukosana na mumewe wakati walipofumaniwa.

Muhtasari

•Kelvin Wambura  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na Bwana Bruno ambaye alimfumania na mke wake kitandani usiku.

•Gidi alikatiza Patanisho hiyo kwani jamaa huyo alisikika kana kwamba anajivunia kitendo chake.

Image: RADIO JAMBO

Kelvin Wambura  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na Bwana Bruno ambaye alimfumania na mke wake kitandani usiku.

Kelvin alidai kwamba mke wa Bruno alikuwa ametorokea kwake usiku baada ya kukosana na mumewe wakati walipofumaniwa.

"Tulikuwa na uhusiano na mke wa Bruno miaka kama mbili nyuma. Tukaendelea hivyo hivyo mpaka huyo jamaa akaja kugundua. Sasa juzi juzi hapa, walikosana na huyo bibi yake halafu akanipigia simu akaniambia nimchukue akuje kwangu," Kelvin alisimulia.

Aliendelea, "Mimi nilikuwa nakula. Akakuja kwa nyumba. Tukakaa nje kidogo mpaka muda wa saa nne nikamwambia twende kwa nyumba, tukafunga mlango. Nilidhani hakuna mtu anaweza kuja hayo masaa, kumbe jamaa alikuwa anamtafuta mke wake.

Ilikuwa ni wakati huo ambapo Gidi alikatiza Patanisho hiyo kwani jamaa huyo alisikika kana kwamba anajivunia kitendo chake na pia kwa sababu ilikuwa kesi kubwa ambayo haingeweza kushughulikiwa wakati wa shoo hiyo ya asubuhi.

Katika Patanisho ya pili ya siku, Sammy Juma (24) kutoka Bungoma aliomba apatanishwe na mke wake Diana (20) ambaye alimuacha mwezi uliopita kwa sababu ya ulevi.

Juma alisema ndoa yake ya miaka miwili ilivunjika baada ya kwenda nyumbani akiwa amelewa na kutaka kumpiga mkewe.

"Nilienda nikakaa kwa wazee nikaonjako kidogo. Vile nilirudi nyumba nikawa nimelewa. Bibi akaleta kisirani. Nilikuwa nataka kumpiga lakini sikumpiga. Baadae tukaenda tukalala lakini hata hatukuongea. Asubuhi nilipoamka nikitaka kuenda kunywa cha sikuona mtu kwa kitanda, nilikuwa tu pekee yangu,"  Juma alisema.

Alieleza kuwa alipofuatilia aligundua kuwa mkewe alikuwa ameenda kwao.

"Nimeacha pombe wiki mbili imeisha. Alienda hivyo na mimi nikabadilika. Siwezi kulewa tena," alisema Juma.

Diana alipopigiwa simu hawakuweza kuwasiliana kwani tayari Juma alikuwa amepanda matatu na kelele zilikuwa nyingi.

Baada ya kuombwa kushuka kwenye matatu, Juma alisemaNimekalia kitu cha nyuma na dere anaendelea tu!"

Mtangazaji wetu Gidi hangeweza kuendeleza Patanisho hiyo kwani mawasiliano yalishindikana kabisa.