Patanisho: Mke abeba picha za mumewe baada ya kutengana, jamaa ashindwa kupata mpenzi mwingine

"Kama amemove on anirejeshee picha zangu, kama hajamove on akuje tulee watoto," Bw Oluku alisema.

Muhtasari

•Oluku alifichua kwamba ndoa yake ya miaka 12 ilisambaratika mwaka wa 2020 baada ya mkewe kumshtumu kuenda nje ya ndoa.

•Sylvia alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba tayari yuko kwa ndoa nyingine na hata amezaa mtoto na mumewe mpya.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Bw Charles Oluku ,35, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Sylvia Naliaka ,28, ambaye alimuacha miaka mitatu iliyopita.

Oluku alifichua kwamba ndoa yake ya miaka 12 ilisambaratika mwaka wa 2020 baada ya mkewe kumshtumu kuenda nje ya ndoa.

"Wakati wa Corona, wakati mwingine nilikuwa nalala nje. Akaanza kunishuku nalala nje kwa wanawake. Pia alilalamika kwamba nakunywa pombe na sikuwa na nia mimi kama hiyo. Huwa tunawasiliana kwa simu," alisema.

Oluku alilalamika kwamba wakati mkewe alipotoroka alibeba watoto wao watatu pamoja na picha zake kadhaa, hatua ambayo alidai huenda imemsababishia masaibu mengi ambayo anakabiliana nayo leo.

"Alienda na picha zangu. Hata sijui kitu alienda kufanyia.Tangu siku hiyo sijawahi kuwa na mpenzi. Roho imekataa tu. Sijui kama alipeleka kwa maombi ya ushirikina. Nataka kujua kama amesonga mbele na maisha yake," alisema.

Alisema kwamba mzazi huyo mwenzake amekataa kurudi kwenye ndoa yao na kusema atakaa na watoto hadi watimize miaka 18.

"Kama amemove on anirejeshe picha zangu, kama hajamove on akuje tulee watoto. Sijawahi kufanya uchunguzi kama ameolewa kwingine lakini huwa tunaongea tu kwa simu," alisema.

Sylvia alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba tayari yuko kwa ndoa nyingine na hata amezaa mtoto na mumewe mpya.

"Anajua mimi nishaolewa. Apeleke ujinga wake mbali. Tayari niko kwa ndoa na niko na mtoto. Anajua hayo," alisema.

Oluku hata hivyo alikana kuwa na ufahamu kwamba mke huyo wake wa zamani ameolewa na mwanaume mwingine.

Bi Sylvia hata hivyo alikata simu, ishara wazi kwamba hana nia ya kurudiana na mzazi huyo mwenzake.

"Sasa angenirudishia picha zangu. Naumia, kupata mtu mwingine ni shida. Hata nimejaribu kuenda kwa makanisa mbalimbali. Nashuku ni juu ya hizo picha, nateseka. Mbona anakatalia picha zangu kama ameoleka," Oluku alisema.

Aliongeza, "Nilikuwa nampenda. Akae na watoto wake vizuri. Sina ubaya na yeye lakini picha zangu atumane. Picha zilikuwa albamu."

Je, ushauri wako ni upi kwa wawili hao?