Patanisho: Mwanadada akataa kurudi baada ya kwenda matanga, amwambia mumewe aoe mwingine

Nduguye Irene alidokeza kwamba Mike alikuwa akicheza karata nje ya ndoa yao ya miaka sita.

Muhtasari

•Mike Baraza ,36, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Irene Baraza ,34, ambaye alitoroka mwezi Januari.

•Joseph alimshauri Mike apige hatua ya kuenda nyumbani kwao ili waweze kushiriki kikao na familia na kutafuta suluhu ya mzozo wao.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mike Baraza ,36, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Irene Baraza ,34, ambaye alitoroka mwezi Januari.

Mike alisema mkewe aliondoka kwenda matanga ya shangazi yake nyumbani kwao ila hajawahi kurudi miezi mitano baadaye.

"Sikuwahi kumkosea. Alisema anaenda matanga kwao. Dada ya mamake alikuwa ameaga. Nilikuwa na shughuli nikampatia nauli na pesa kidogo akaenda," Mike alisema.

Alisema kila anapompigia mkewe simu amekuwa akimwambia atafute mke mwingine.

"Nikimpigia simu anasema tu nione mke mwingine. Sijui shida ni nini. Aliondoka tu akaenda sijui shida ni nini," alisema.

Mtangazaji Ghost Mulee alipopiga namba ya Irene, aliyepokea simu ni ndugu yake mdogo Joseph ambaye alidai dadake aligura ndoa yake ya miaka sita kutokana na tabia ya Mike ya kuwa na mipango wa kando.

"Irene alitoka huko kwako na akaleta malalamishi huku nyumbani. Anasema wewe unaonekana mjanja. Kuna vile hamuishi kama mke na mume hapo nyumbani," Joseph alimwambia shemeji yake Mike.

Joseph alimshauri Mike apige hatua ya kuenda nyumbani kwao ili waweze kushiriki kikao na familia na kutafuta suluhu ya mzozo wao.

"Wanafaa wakae  chini waongee. Kama kutakuwa na suala nzito, waite familia waongee," Joseph alisema.

Mike alimwambia Joseph, "Akija mwambie mimi bado nampenda. Mimi sina mpango wa kando. Nataka arudi tuendelee kulea watoto pamoja."