Patanisho: Ndoa ya miaka 17 yavunjika baada ya mume kupata ajali, kuvunjika mguu

Musa alisema mkewe alikuwa na mpango wa kuenda Qatar kwa ajili ya kazi, jambo ambalo hakupendezwa nalo.

Muhtasari

•Musa alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 17 baada ya yeye kuhusika katika ajali takriban miezi miwili iliyopita.

"Ata siongei kuhusu hiyo stori. Hiyo stori sitaki kuongelea sana. Wacha ipotelee mbali," Maureen alisema kisha akakata simu.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanaume aliyejitambulisha kama Musa Mengich ,40, kutoka kaunti ya Baringo alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Maureen Ruto ,32, ambaye alitoroka hivi majuzi.

Musa alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 17 baada ya yeye kuhusika katika ajali takriban miezi miwili iliyopita.

Alisema kwamba mkewe alikuwa na mpango wa kuenda Qatar kwa ajili ya kazi, jambo ambalo hakupendezwa nalo.

"Wakati nilikuwa nafanya kazi, nilikuwa naenda Pokot nikapata ajali mnamo Aprili 14. Kuna mahali nilipata wavamizi kwa barabara nikiwa na pikipiki nikashtuka nikaanguka nikavunjika mguu," Musa alisimulia.

Aliongeza, "Niliambiwa niende Hospitali ya Kijabe nikakosa pesa. Nilikaa tu nyumbani na mke wangu. Kumbe bibi alikuwa na mpango wa kuenda shule Nairobi, baada ya shule aende Qatar. Ilifika mahali akaniambia anataka kuenda Qatar, nikakataa. Saa hii sijui mahali ako, hachukui simu zangu. Amechukua watoto wawili wadogo, mwingine ako shule na mimi niko na wawili nyumbani. Anaambia watu eti nilikataa aende masomo, akaona ajipange aende Qatar.Ni ngumu  kukaa nyumbani kama sijui ako wapi. Alikuwa ameniambia kuhusu mpango wa kwenda Qatar kitambo nikadhani ni mzaha."  

Maureen alipopigiwa simu, alikataa kabisa kuzungumzia masuala yake na mumewe.

"Ata siongei kuhusu hiyo stori. Hiyo stori sitaki kuongelea sana. Wacha ipotelee mbali," Maureen alisema kisha akakata simu.

Musa alisema, "Alitoka Ijumaa. Hakuna kitu ingine nilimfanyia. Kuna siku niliongea vibaya, baadaye nikaenda kanisani nikaomba msamaha."

Je, una ushauri ama maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?