Patanisho: Sitaki mtoto wangu alelewe na baba mwingine- Jamaa alalamika

Muhtasari

•Douglas alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili akiwa kufuatia mzozo wa kinyumbani.

•Alisema hajawahi kumuona mpenzi huyo wake wala mtoto wao wa mwaka mmoja tangu alipozaliwa mapema mwaka jana.

Ghost Mulee studioni
Ghost Mulee studioni
Image: RADIO JAMBO

Douglas Omurwa alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mpenzi wake Mercy Kiprono ambaye alitengana naye mwaka jana.

Douglas alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili akiwa kufuatia mzozo wa kinyumbani. Alifichua kuwa Mercy alikuwa mjamzito wakati alipoondoka.

"Tulikuwa tunaishi naye kuanzia 2019-2021 nikatoka kidogo nikaenda kazi Bungoma. Kurudi sikumpata kwa nyumba. Alikuwa kwa jirani nikaenda nikampata tukakorofisha kidogo. Alikasirika kisha siku iliyofuata akaenda," Douglas alisema.

Douglas alifichua kuwa baadae mkewe alijifungua na akamfahamisha kupitia simu ila hakuenda kuona mtoto wao. 

Alisema hajawahi kumuona mpenzi huyo wake wala mtoto wao wa mwaka mmoja tangu alipozaliwa mapema mwaka jana.

"Alijifungua na akanipigia simu akaniambia niende hospitali lakini sikuwa na pesa singeweza kuenda. Baada ya kujifungua alihama kutoka mahali alikuwa anaishi. Sasa naishi na hofu kuhusu mtoto wangu," Alisema Douglas.

"Sijawahi kumtumia pesa za matumizi ya mtoto. Huwa nataka kumtumia lakini huwa ananipatia majibu mabaya," 

Mercy alipopigiwa simu alitupilia mbali madai ya Douglas kuwa amekuwa akizungumza naye katika juhudi za kutafuta suluhu.

Alisema Douglas hajawahi kumtumia chochote na kufichua kuwa tayari alikuwa anapanga kuelekea mahakamani kumshtaki kwa kutelekeza mtoto wao.

"Mbona hujawahi kusaidia mtoto? Mimi nilikuwa nafikiria ushaoa. Mimi nilikuwa nimesema nakushtaki," Alisema.

Alisema, "Hajawahi kuzungumza nami. Hakuna chenye amenisaidia nacho kabisa."

Douglas aliomba msamaha na kumsihi mama huyo wa mtoto wake akubali warudiane ili waweze kulea mtoto wao pamoja.

"Sitaki mtoto wangu alelewe na baba mwingine. Niko tayari kukuoa na kukupeleka nyumbani," Alisema.

Mercy hata hivyo alisema hayupo tayari kurudiana na Douglas huku akidai kuwa ameteseka sana kwa ajili yake.

"Asaidie mtoto pekee yake lakini uhusiano sitaki. Amenitesa ya kutosha. Kurudiana itakuwa ngumu," Alisema.

Douglas alilazimika kukubali uamuzi wa Mercy na akaahidi kuwa anatuma pesa za matumizi ya mtoto.