AFCON: Mali walima Mauritania 4-1, Angola walazimisha sare dhidi ya Tunisia

beIN SPORTS
beIN SPORTS
Mali waliwacharaza magwiji Mauritania mabao 4-1 na kupanda kileleni mwa kundi E jana usiku, michuano ya mwaka huu ya AFCON ilipoingia siku ya nne nchini Misri.

Abdulahi Diabi alianza kufunga mabao kabla ya Moussa Marega na Adama Traore kufanya mambo kuwa mabao matatu. Mauritania walipata bao la kufuta machozi kupitia kwa El Hasen katika dakika ya 72 kupitia mkwaju wa penalti, kabla ya Traore kufunga bao la nne.

Wakati huo huo, Djalma alisawazisha bao la Youssef Msakni katika kipindi cha kwanza na kuipatia Angola sare ya 1-1 dhidi ya Tunisia katika kundi E.

Awali bao la pekee la Jonathan Kodjia liliisaidia Ivory Coast kuwanyuka Afrika Kusini 1-0 katika mechi yao ya ufunguzi ya kundi D na kupanda kileleni na Morocco baada yao kuwanyuka Namibia Jumapili.

Cameroon wataanza kutetea taji lao la Ubingwa bara Afika nchini Misri hii leo dhidi ya Guinea Bissau kuanzia saa mbili usiku huku kipute hicho kikiingia siku yake ya tano nchini Misri.

Kocha mpya Clarence Seedorf atazikosa huduma za kiungo Joel Tagueu ambaye alipatikana na ugonjwa wa moyo, pamoja na mshambulizi Vincent Abubakar kutokana na jeraha.

Miamba hao almaarufu Indomitable Lions wataongozwa na kocha Mholanzi Clarence Seedoff kwa mara ya kwanza huku mshambulizi Eric Maxim akiwa nahodha. Mechi ya mwisho ya makundi itakua kati ya Ghana na Beninn saa tano usiku.

Kwingineko, aliyekua kiongozi wa IAAF Lamine Diack, na mwanae Papa Diack watakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na ulaghai wa pesa nchini Ufaransa.

Diack alikua rais wa IAAF kati ya mwaka 1999-2015 lakini utawala wake ulighubikwa na utata na madai ya ufisadi. Diack mwenye umri wa miaka 86 ambaye amekua katika kifungo cha nyumbani nchini Ufaransa na mwanae, wanashtumiwa kwa kuzuia marufuku ya utumizi wa dawa zilizoharamishwa kwenye spoti dhidi ya Urusi.