Aguero apeperusha Man City huku Newcastle wakiwaadhibu Tottenham

newcastle
newcastle
Mabao mawili ya Sergio Aguero na Raheem Sterling yaliwasaidia Manchester City kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Bournemouth. Aguero alianza kufunga kunako dakika ya 14 kabla ya Raheem Sterling kuongeza la pili dakika mbili baadae.

Bournemouth walipata bao la kufuta machozi baada ya Harry Wilson kufunga bao na kufanya mambo kuwa 2-1. Aguero kisha akaonyesha ujuzi wake tena na kuongeza bao kunako dakika ya 64.

Matokeo haya yanawapandisha City hadi katika nafasi ya pili kwenye jedwali alama mbili nyuma ya mahasimu wao wa msimu uliopita Liverpool.

Bao la kwanza la Joelinton katika soka ya Uingereza liliwapa Newcastle ushindi wa kushangaza dhidi ya Tottenham na kumpa Steve Bruce alama zake za kwanza kama meneja wao.

Mshambulizi huyo raia wa Brazil alichukua fursa ya kusitasita kwa ulinzi wa Tottenham na kufunga bao. Spurs hawakuwa na ubunifu wa kuvunja ari ya Newcastle ambao walijizatiti kushinda mechi hio.

Inter Milan imefungua mazungumzo na Manchester United kuhusu kiungo wa Chile Alexis Sanchez, mwenye umri wa miaka 30, na wanataka kukamilisha mkataba wa mkopo katika siku tatu zijazo.

Kwingineko Barcelona imewasilisha ombi jipya kwa mshambuliaji kiungo wa Paris St-Germain na wa timu ya taifa ya Brazil Neymar, mwenye umri wa miaka 27, linalojumuisha fedha zaidi na wachezaji zaidi.

Antoine Griezmann alianza mechi yake ya kwanza Barcelona kwa kufunga mabao mawili walipowanyuka Real Betis katika La Liga. Griezmann, aliyesajiliwa Julai kwa kitita cha pauni milioni 107, alisawazisha bao la ufunguzi la Nabil Fekir, na kisha kuongeza lingine dakika tano baada ya muda wa mapumziko.

Carles Perez alifungia Barca bao la tatu.  Jordi Alba na Arturo Vidal walifanya mabo kuwa 5-1 kabla ya bao la Loren. Griezmann, aliyesajiliwa kutoka Atletico Madrid, alikuwa chini ya shinikizo kubwa la kuonyesha mchezo mzuri baada ya kuanza vibaya dhidi ya Bilbao.

Jitihada za Kenya kutafuta medali zaidi katika mshindano yanayoendelea ya All Africa games zitaendelea hii leo katika michezo mbalimbali. Mbio za wanaume za mita elfu 3 kuruka viunzi na fainali ya mbio za mita elfu 5 kwa kinadada zitaangaziwa leo.

Katika mbio za wanaume kuruka viunzi bingwa wa dunia na olimpiki Conseslus Kipruto anatarajiwa kuongoza jitihada za Kenya za medali ya dhahabu akisaidiwa na Benjamin Kigen na Joash Kiplimo.

Lydia Jeruto na Lilian Kasait watatafuta meadli katika mbio za kinadada saa tatu usiku wa leo.