Atletico Madrid yaishutumu Barcelona kwa 'utovu wa heshima'

Atletico Madrid imeshutumu Antoine Griezmann na Barcelona kwa 'utovu wa heshima' na kusema mabingwa hao wa La Liga walizungumza na mchezaji wa kiungo cha mbele wa timu hiyo mnamo Machi.

Atletico inasema imekataa ombi la Barcelona na kumuagiza Griezmann arudi kwa mazoezi ya kabla kuanza kwa msimu.

Katika taarifa yake timu hiyo ya Madrid imeelezea "kushutumu vikali tabia ya pande zote mbili, hususan kwa Barcelona".

Griezmann, mwenye umri wa miaka 28, mnamo Mei alisema ataondoka Atletico msimu huu wa joto.

Raia huyo wa Ufaransa amefunga mabao 94 katika La Liga katika mechi 180 za Atletico na anatarajiwa na wengi kuhamia Barcelona.

Mkataba wake umemfunga kwa thamani ya Euro milioni 120 lakini Atletico inasema wapinzani wake wa La Liga wanataka kuahirisha malipo na wameanza kuzungumza na yeye miezi kadhaa iliyopita.

"Ni wazi, Aletico ilikataa. Inaeleweka kwamba Barcelona na mchezaji mwenyewe waliivunjia Atletico heshima na mashabiki wake wote," taarifa ya Atletico imeongeza.

'Hatuwazungumzii wachezaji wengine'

Mapema hapo jana Ijumaa, rais wa Barca Josep Bartomeu amesema klabu hiyo iliwasiliana na Griezmann na kwamba mchezaji wake wa zamani wa kiungo cha mbele Neymar "anataka kuondoka Paris St-Germain".

Mchezaji wa kimataifa raia wa Brazil Neymar aliondoka Barcelona kuelekea PSG mnamo 2017 kwa kitita kilichoweka rekodi cha thamani ya Euro milioni 222 na inaarifiwa huenda atarudi.

Bartomeu amesema anafahamu pia mahali ambapo mlinzi mwenye miaka 19 wa Uholanzi Matthijs de Ligt, anaelekea wapi msimu ujao. Amehusishwa na uhamisho kwenda Ajax.

Tayari Barcelona imemsajili mchezaji mwenza wa De Ligt katika timu ya kimataifa Frenkie de Jong kutoka mabingwa hao wa Uholanzi.

"Tumewasiliana kwa mara ya kwanza na Griezmann jana," Bartomeu alisema jana Ijumaa "Kuna hamu na ndio maana tulikutana.

"Huwa hatuwazungumzii wachezaji kutoka timu nyingine.

"Tunafahamu kuwa Neymar anataka kuondoka PSG lakini tunajua kuwa PSG haimtaki Neymar aondoke.

"Nilisema tangu kitambo nafahamu mahali atakapocheza De Ligt . bado nalijua hilo na siwezi kusema zaidi ya hilo."

Wakati wa kuzinduliwa De Jong, Bartomeu aliulizwa kuhusu taarifa ya Atletico'akiongeza: "Tunamuidhinisha De Jong na nitalizungumzia hilo wakati mwingine."