Buriani Walibora, kwa wapenzi wa Kiswahili nyota yako itang'aa daima

kidagaa
kidagaa
Na Sairin Lupia

Kwa maneno ya Kongewea Mswahili, ‘basi hiyo itakuwa siku njema’ lakini leo si njema siku bali majonzi tele kwa kumpoteza mwandishi bora walibora. Jina na sifa za Ken Waliaula Walibora vitasalia katika nakala za kumbu kumbu hasa katika fani ya uandishi nchini Kenya na dunia nzima.

Ken walibora amekuwa mwandishi wa kuigwa na kutumiwa kama mfano kwa waandishi wengine wanaochipukia.

Vitabu vyake vimekuwa vyenye simulizi za kuburudisha na kuelimisha na kuafikia malengo ya fasihi andishi. Katika vitabu vyake amegusia mada kadha wa kadha na kudhihirisha ukwasi wake katika uandishi.  Alikuwa na ustadi wa kipekee kutumia wahusika kusimulia hadithi zake. Marehemu Walibora kupitia kazi yake ya uandishi amenata nyoyo za wengi katika kukuza maadili mema katika jamii ambayo kwangu binafsi yamenihamasisha pakubwa na kunipa mwongozo mahsusi maishani.

Amegusia mada kama ukoloni mamboleo, uongozi mbaya katika bara la afrika; mkoloni mzungu aliondoka na kuingia mkoloni mweusi. Amezungumzia umuhimu wa wanawake katika ukombozi na pia katika jamii. Kupitia wahusika kama vile Kongowea Mswahili alitufunza maadili kama ya kuwa mtu mwenye bidii na umuhumi wa familia.

Ukifuatilia maisha ya mhusika huyu katika kitabu alichokiandika kwa ufasaha ‘Siku njema’, basi utaona mateso alioyapitia kijana huyu katika safari yake kutoka Tanzania hadi Kenya, Kitale akimsaka babake mzazi.

Ni uandishi kama huu wa hadhi ya juu uliochangia kukubaliwa kwa vitabu vyake hadi kutumika katika mtaala wa shule za upili. Vitabu vyake vimetahiniwa katika mitihani ya kitaifa ya shule za upili kwa miaka mingi sasa. Kitabu cha Kidaagaa Kimemwozea, ambacho nilikifanya kwa fasihi katika shule ya upili, ni miongoni mwa vitabu vyake vilivyomletea sifa kede kede. Kitabu chake cha hadithi fupi, Nizikeni papa hapa, kilicho katika Tumbo Lisiloshiba na hadithi zinginezo ni moja wapo wa vitabu vya fasihi vinavyosomwa katika sekondari kwa wakati huu.

Kwa hakika Ken Walibora alikuwa mwandishi wa kuigwa. Kitabu chake cha kwanza kukisoma kilikuwa Ndoto Ya Amerika. Katika simulizi hii, Ken anatuonyesha kwamba watu wengi hasa kutoka Afrika huwa na ndoto ya kwenda Amerika. Lakini anatukumbusha kwamba kwetu sisi waafrika Amerika yetu ni papa hapa nyumbani. Tuishi hapa Afrika tuendeleze bara letu na nchi zetu ili tuishi maisha yenye starehe na raha kama mambo yalivyo kule Amerika.

Walibora alikuwa na ustadi wa kipekee katika kutumia mbinu za uandishi kama vile kinaya, semi, methali, misemo, tashhisi, tashbihi na mbinu zinginezo. Ustadi huu ulivutia sana wasomaji wa hadithi zake. Uongozi wa Mtemi Nasaba Bora, jina lake likiwa kinaya, ama alivyopenda kumwita mhusika mmoja, Mtemi Nasaba Mbaya Mbovu, ni mfano maalum wa uongozi katika bara letu tangu jadi. Jinsi viongozi wetu wanavyotumia vyeo vyao kujifaidisha huku wananchi wengi wakiishi kwa uchochole, ama kama anavyosema Pauline Keya , “wala kuku na wenzako wala kama kuku”.

Alituonyesha jinsi vyongozi wanavyopata mamlaka kupitia njia za mkato, na wanavyo fuja pesa za umma ambazo zingetumika katika kujenga hospitali na zahanati. Viongozi kama hawa bado wangalipo katika Afrika huru na nchi hata za ng’ambo.

Ken alituonyesha umuhimu wa urafiki katika kitabu chake cha Kufa kuzikana. Maadili yaliyomo katika vitabu vya Ken walibora ni chungu nzima na kuyazungumzia yote kwa sasa kitakuwa kibarua kigumu. Wahusika wote katika vitabu vyake walikuwa na ujumbe wa kupitisha kwa jamii, kutoka kwa Otii na Rehema wanjiru, Selemani Mapunda na Athman, Mwalimu Majisifu na Majununi (Major Noon), hadi kwa Issa, wote wanaumuhimu katika fasihi andishi ambayo ni kioo cha jamii.

Shujaa, gwiji, mwanahabri, mwalimu na mwandishi tajika Ken Walibora atakumbukwa daima na kazi yake itasalia iking’aa hata ingawa yeye mwenyewe atakuwa ameondokea dunia. Kazi yake itasalia kigezo katika uandishi wa vitabu. Kama anavyosema katika kitabu chake, hata nikifa kuzaliwa matuko weye wengine, basi akifa kuna matumaini kwamba kutazaliwa Ken walibora wengine watakao peleka Kiswahili mbele.

Tutamkumbuka milele daima na atabakia kuwa shujaa katika kupigania nafasi ya Kiswahili katika nyanja muhimu duniani. Hivyo basi litabaki kuwa jukumu letu kutomzika Walibora nyoyoni mwetu bali kuhaisha kazi yake ya uandishi na kudumisha jumbe zake kwetu sisi alizotoa kupitia uandishi wake.

Mwandishi Sairin Lupia ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.