Gavana Sakaja azungumzia suala la kupatia barabara jina la marehemu E-sir

Seneta huyo wa zamani alielezea hamu yake ya kuona ombi hilo likitimizwa.

Muhtasari

•Huku akijibu pendekezo hilo, gavana Sakaja alibainisha kuwa itakuwa furaha yake kuona jambo hilo likitimia. 

•Hata hivyo aliweka wazi kuwa taratibu zote za kisheria lazima zifuatwe kabla ya hilo  kutekelezwa.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na marehemu E-sir
Image: HISANI// FACEBOOK

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja hatimaye amevunja kimya kuhusu suala la kupatia barabara moja la jiji jina la marehemu Issah Mmari Wangui almaarufu E-Sir.

Mapema wiki hii msanii Nameless alianzisha ombi la kutaka barabara moja katika mtaa wa South C kupewa jina la marehemu mwenzake na rafikiye mkubwa.

Mwimbaji huyo mkongwe alibainisha kuwa  E-sir ameendelea kuhamasisha kizazi kipya licha ya kuaga kwake takriban miongo miwili iliyopita.

"Jina la Esir linaendelea kuhamasisha kizazi kipya na kupatia barabara jina lake kutasherehekea urithi wake wa talanta, bidii, shauku na unyenyekevu . Pia kutasisitiza umuhimu wa sanaa katika utamaduni wetu," Nameless alisema kupitia Facebook.

Aliwaomba wanamitandao kutia saini kwenye ombi hilo ili kushinikiza serikali kuchukua hatua hiyo.

Huku akijibu pendekezo hilo, gavana Sakaja alibainisha kuwa itakuwa furaha yake kuona jambo hilo likitimia. 

"Mimi mwenyewe nimekuwa msanii na E-sir alikuwa rafiki yangu.Nilikuwa namjua, najua ndugu yake Habib na familia yake. Pia mimi nimeishi pale South C. Ni jambo la busara kuwakumbuka wasanii wetu. Yeye alibobea sana kwa hiphop, alikuwa mmoja wa waanzilishi," alisema katika mahojiano na Mwalili TV.

Seneta huyo wa zamani alielezea hamu yake ya kuona ombi hilo likitimizwa.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa taratibu zote za kisheria lazima zifuatwe kabla ya hilo  kutekelezwa hatimaye.

"Lazima umma ushirikishwe. Lazima hoja iletwe kwenye bunge la kaunti. Hatua hiyo tutafuata. Kwangu mimi ni jambo ambalo nitafurahia,"

Sakaja alidokeza kuwa taratibu hizo huenda zikachukua miezi kadhaa kabla ya kukamilika na ombi kutekelezwa.

"Hakuna haraka. Tunataka kumkumba katika siku za usoni. Sio jambo la kuharakisha, ni jambo la kufanya vizuri,"

E-sir alifariki mnamo Machi 13, 2003 kufuatia ajali mbaya ya barabara iliyotokea  katika barabara ya Nakuru- Nairobi.

Alikuwa na umri wa miaka 21 tu wakati alipokumbana na kifo chake.