Sonko ataka watu wamuombee aache pombe, apakia video ya Ruto akiimba

Mfanyabiashara huyo aliotoa maoni yake na kusema kuwa ameguswa na alichofanya Rais

Muhtasari

• Tajiri huyo aliwataka wafuasi wake pia kumtia katika maombi ili naye apate kuokoka na kuacha kutumia pombe.

Sonko amesema ikulu imebadilika na kuwa sehemu takatifu
Sonko amesema ikulu imebadilika na kuwa sehemu takatifu
Image: Instagram

Sonko alisema kwa mshangao kuwa Rais wa sasa ameweza kuibadilisha ikulu ikawa mahali pa maombi,

Kiongozi huyo alipakia video ya rais Ruto akifanya ibada kwenye ikulu huku akiwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiimba kwa kusujudu.

Tajiri huyo aliwataka wafuasi wake pia kumtia katika maombi ili naye apate kuokoka na kuacha kutumia pombe, kwa kusema kwamba baada ya kupata wokovu atakuwa anakunywa kidogo kama Yesu.

"Niombeeni niwache pombe na kama ni kukunywa niwe nakunywa kidogo kidogo kama ile mvinyo ambayo Yesu alikuwa anakunywa. Yuko Mungu mbinguni asikuaye maombi," Sonko aliandika kwa utani wa aina yake.

Sonko anatoa matamshi haya siku moja tu baada ya rais Ruto na familia yake kuandaa ibada kubwa kabisa katika ikulu ya Nairobi ambapo aliwarai viongozi hao wa kanisa kuzidi kuliweka taifa mikononi mwa bwana.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa kanisa zaidi ya 40 ilikuwa pia imeandaliwa kuuombea uchumi na migororo ambayo imekuwa ikikumba taifa la Kenya.

"Nawataka muombee amani ya nchi yetu. Kenya ni nchi tegemeo. Nilizungumza na viongozi wengi kwa muda wa wiki kadhaa zilizopita na wanaangalia Kenya ili kutoa suluhu kwa amani ya eneo letu. Kutoka Somalia hadi Ethiopia. Hadi DRC ,Sudan Kusini na eneo lote hili,” alisema.

Mama wa Taifa Rachel Ruto pia aliongelea suala hilo la kutakasa Ikulu.

Alisema kuwa Ikulu itakuwa mahali pa maombi ambapo ibada itakuwa ikiandaliwa kila mwezi kwa minajili ya kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu.

Ibada hiyo iliyoandaliwa katika Ikulu ya Nairobi ndiyo ya kwanza kufanyika kutoka uapisho wake Rais na baada yake kuhamia kule Ikuluni. Iliwakutanisha viongozi mbali mbali wa Kikristo waliojumuika kufanya maombi maalum.