Eric Omondi aachiliwa baada ya kuzuiliwa na polisi kwa saa kadhaa

Ilikuwa ni mara yake ya tatu kukamatwa katika kipindi cha miezi miwili.

Muhtasari

•Hapo awali Eric Omondi alikamatwa mara mbili kuhusiana maandamano dhidi ya gharama ya maisha.

•"Nasikia vizuri sana niko free" alisema

Mchekeshaji Eric Omondi aliachiliwa kutoka kwa kizuizi cha polisi siku ya Jumatatu jioni baada ya kuzuiliwa kwa saa kadhaa kufuatia kukamatwa kwake akipeleka CVs Ikulu.

Ilikuwa ni mara yake ya tatu kukamatwa katika kipindi cha miezi miwili. Hapo awali alikamatwa mara mbili kuhusiana maandamano dhidi ya gharama ya maisha.

Kukamatwa kwa Jumatatu kulikuja baada ya mchekeshaji huyo kunaswa akivuta 'mkokoteni' aliodai kuwa na maelfu ya CV za vijana wanaotafuta kazi.

Alikamatwa kwenye Barabara Kuu ya Uhuru alipokuwa akienda kupeleka hati hizo katika Ikulu, eneo lililozuiliwa na makazi rasmi ya rais.

"Nasikia vizuri sana niko free" alisema baada ya kutoka nje ya Kituo Kikuu cha Polisi.

Katika video iliyochapishwa na mtayarishaji wa maudhui Vincent Mboya, Omondi alionekana akifuatwa na  mfanyibiashara Gor Semelang'o hadi kwenye Ukumbi wa Kitaifa wa Kenya umbali wa mita chache.

Alisema ni lazima apeleke CV hizo mahali alipopangiwa siku ya Jumatano.

“Hizo ma-CV, tutazipeleka (Lazima tufikishe hizo CV),” alisema.

Mchekeshaji huyo aliyegeuka kuwa mwanaharakati alikamatwa kwa mara ya kwanza Februari 21 kwenye Njia ya Bunge alipokuwa akiongoza maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.

Alikamatwa pamoja na wengine 17 na baadaye kushtakiwa kortini kwa mkusanyiko usio halali. Kesi hiyo itasikilizwa mwezi Mei.

Omondi alikamatwa tena Machi 1 alipokuwa akisambaza unga wa mahindi kwa wafuasi wake katika uwanja wa City Stadium jijini Nairobi.

Aliachiliwa bila masharti mnamo Machi 6.