Diamond ajawa bashasha baada ya Zari kumtembelea wiki moja tu baada ya kufunga ndoa

Ziara hii inakuja siku chache tu baada ya Zari kuvishwa pete ya ndoa na mchumba wake, Shakib Cham Lutaaya.

Muhtasari

•Wakati akiwapeleka nyumbani baada ya kuwalaki katika uwanja wa ndege, Diamond alionekana kufurahi sana kuona familia yake tena. 

•Mwanasosholaiti huyo wa Uganda hakuonekana kwenye Roll Royce walilopanda watoto kutoka uwanja wa ndege.

Diamond, Prince Nillan, Zari Hassan na Tiffah Dangote
Image: HISANI

Mwanasosholaiti wa Uganda Zari Hassan na watoto wake wawili wadogo, Tiffah Dangote na Prince Nillan wanaaminika kuwa nchini Tanzania.

Watatu hao wanaripotiwa kutua katika nchi hiyo jirani siku ya Ijumaa usiku na kupokelewa na staa wa Bongo Diamond Platnumz pamoja na Iddy Santos. Inaaminika kuwa dhumuni la ziara hiyo ni Tiffah na Nillan wapate kusherehekea Eid pamoja na baba yao Diamond na familia yake nyumbani kwake katika jiji la Dar es Salam.

Wakati akiwapeleka nyumbani baada ya kuwalaki katika uwanja wa ndege, Diamond alionekana kufurahi sana kuona familia yake tena. Huku akirekodi, aliwaomba watoto wake wawasalimie Watanzania na kuwajulisha kuhusu ziara yao.

"Babaa (Nillan). Isalimie kamera. Sema hello Tanzania, tuko hapa kutoka Afrika Kusini," Diamond aliwaambia huku wakirudia maneno yake.

Aliendelea kusema, "Tiffah yuko hapa. Unaendeleaje kipenzi (Tiffah)." huku akimuonyeha binti yake kwenye kamera.

Tiffah na Nillan hata hivyo hawakuonekana wachangamfu, labda kutokana na uchovu wa safari ya kutoka Afrika Kusini hadi Tanzania.

Diamond pia hakumuonyesha mzazi mwenzake Zari Hassan kwenye kamera na kwa kuangalia video aliyochapisha, mwanasosholaiti huyo wa Uganda aidha alitumia gari lingine kutoka uwanja wa ndege kando na Roll Royce walilopanda watoto, ama alisalia Afrika Kusini na hakufika nao nchini Tanzania.

Ziara hii inakuja siku chache tu baada ya Zari kufunga pingu za maisha (Nikah) na mpenzi wake wa mwaka mmoja, Shakib Cham Lutaaya.

Zari Hassan na Shakib walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah wikendi iliyopita baada ya kuchumbiana kwa takribani mwaka mmoja.

Wawili hao walivishana pete usiku wa manane kuamkia Jumatatu katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wapenzi hao walionekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la faraghani, wawili hao ambao wamekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka minne waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.

Hapo awali, Zari alawahi kufichua kwamba alikuja kujuana na Shakib baada ya kutengana na Diamond mwaka wa 2018.