Nimewachoka! Paula ajawa hasira baada ya mahusiano yake na Marioo kukosolewa, awafokea wakosoaji

"Ifike mahala mheshimu maisha ya mtu binafsi, nina haki ya kuwa na mtu nimpendaye," Paula alifoka.

Muhtasari

•Paula amewataka wanaoingilia mahusiano yake kukoma huku akibainisha kwamba wengi wao ni wanawake wakubwa wanaostahiki kuwa mamake.

•Nilimpenda wa kwanza nikamtambulisha tukaachana, mlikuwa mnatakaje? Nisidate tena? Au nisidate kisirisiri?," alihoji.

Marioo na mpenzi wake Paula
Image: HISANI

Mwanamitindo maarufu wa Tanzania Paula Paul Kajala aliamka akiwa amejawa na hasira siku ya Jumanne asubuhi.

Bila shaka, mlimbwende huyo mwenye umri wa miaka 20 hafurahishwi na watu kuingilia mambo yake hasa mahusiano.

"Ifike mahala mheshimu maisha ya mtu binafsi, nina haki ya kuwa na mtu nimpendaye kama watoto zenu/ndugu zenu/na nyinyi wenyewe mnavyofanya (Tofauti yetu, nyinyi mnafanya gizani mimi ninawaonyesha)," Paula kwa hasira nyingi alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne asubuhi.

Binti huyo wa muigizaji wa filamu bongo Frida Kajala Masanja amewataka wanaoingilia mahusiano yake kukoma huku akibainisha kwamba wengi wao ni wanawake wakubwa wanaostahiki kuwa mamake.

Alihoji jinsi wakosoaji wake wanataka aishi maisha yake kuona kwamba baadhi yao wanapinga hatua zake.

"Wengi ni mama zangu mnaoongea kwa hasira vitu ambavyo siyo vya ukweli. Natumia lugha nyepesi sana, achaneni na maisha yangu.

Nilimpenda wa kwanza nikamtambulisha tukaachana, mlikuwa mnatakaje? Nisidate tena? Au nisidate kisirisiri?," alihoji.

Mwanamitindo huyo anayeaminika kuwa mpenzi wa Marioo aliwataka wakosoaji kuangazia familia zao na kutoingia maisha yake.

"Mungu tu anaweza kunihukumu! Nyie waungu watu wa kwenye mitandao muda huu mngeutumia kuabudu makanisani/ msikitini na mngekuwa mmekokoa roho za watu wengi kuliko hichi mnachokifanya. Nimewachoka," alisema.

Paula alidokeza kuwa baadhi ya wakosoaji walitaka kumuona amehuzunika baada ya kuachana na Rayvanny mwaka jana. Aliendelea kubainisha kwamba anamshukuru Mola kwa kumbariki na kumbariki na bavu lake, Marioo.

"Mniache niishi kwa amani mnitoe kwenye midomo yenu hata  nikiharikiwa nyie inawahusu nini kwa sababu hakuna ata mmoja anayenisaidia mpaka hapa  nilipo. Achaneni na mimi  mfocus na maisha yenu. Maisha yangu yatawasumbua na hakuna cha maana mtakachokipata kwa kuniongelea mimi vibaya," alisema.

Paula alimtambulisha Marioo kama mpenzi wake mpya siku chache tu baada ya aliyekuwa mpenziwe, Rayvanny kuthibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na mzazi mwenzake Fahyma almaarufu Fayvanny.

Hivi majuzi, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 alikiri mapenzi yake yasiyoisha kwa mtunzi huyo wa kibao 'Mi Amor.'

Kwenye akaunti yake ya Snapchat, mpenzi huyo wa zamani wa Rayvanny alibainisha hatimaye amepata mpenzi wa ndoto yake.

Paula aliendelea kubainisha kuwa anafurahia sana mahusiano yake na mwimbaji huyo wa nyimbo za bongofleva.

"Nimepata mwanaume ninayemtaka, nina furaha," alichapisha.

Wawili hao wamekuwa wakionekana pamoja katika siku za hivi majuzi huku mahaba baina yao yakionekana kuendelea kunoga.