Paula amtambulisha mpenzi wake Marioo kwa mama yake Kajala Masanja

Paula alimpeleka Marioo kwa mamake, wakasalimia kwa heshima kabla ya kushiriki mazungumzo.

Muhtasari

β€’Paula aliandamana na anayedaiwa kuwa mpenzi wake, mwimbaji Omary Mwanga almaarufu Marioo kwenye hafla hiyo.

β€’Kajala alionekana mchangamfu na mwenye bashasha tele wakati akicheza na mkwe wake Marioo jukwaani.

Kajala, Paula, Marioo
Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumatano, muigizaji wa filamu bongo Frida Kajala Masanja na binti yake Paula Paul waliandaa hafla ya Usiku wa Paula na Kajala ambapo walizindua rasmi Reality Show yao mpya itakayopeperushwa kwenye Zamaradi TV.

Hafla hiyo ambayo iliandaliwa katika ukumbi wa Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam ilihudhuriwa na makumi ya wageni waalikwa wakiwemo marafiki, wanafamilia na watu wengine mashuhuri katika tasnia ya sanaa ya bongo.

Paula aliandamana na anayedaiwa kuwa mpenzi wake, mwimbaji Omary Mwanga almaarufu Marioo kwenye hafla hiyo. Wakati hafla ikiendelea, wawili hao walionekana wakipiga gumzo, wakicheza na kukumbatiana kimahaba.

Kwa wakati fulani, Paula alionekana akimpeleka mwimbaji huyo kwa mamake Kajala ambaye alimsalimia kwa heshima kabla ya wawili hao kushiriki mazungumzo. Marioo pia aliwatumbuiza wageni kwenye hafla hiyo ambapo muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alijumuika naye kwenye jukwaa ili kucheza pamoja.

"Binadamu ninaowapenda zaidi @kajalafrida @marioo_tz," Paula alisema kuhusu video ya Marioo akicheza na mama yake.

Kajala alionekana mchangamfu na mwenye bashasha tele wakati akicheza na anayedaiwa kuwa mkwe wake jukwaani.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, muigizaji huyo mkongwe alikiri hana uhakika iwapo Marioo na binti yake  yupo wanachumbiana.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize aliweka wazi kuwa pia yeye anapata tetesi za mahusiano ya wawili hao kwenye mitandao ya kijamii.

"Sijui. Kwa kweli sijui chochote. Picha naziona tu kama wananchi wengine," alisema.

Paula alimtambulisha Marioo kama mpenzi wake mpya siku chache tu baada ya aliyekuwa mpenziwe, Rayvanny kuthibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na mzazi mwenzake Fahyma almaarufu Fayvanny.

Hivi majuzi, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 alikiri mapenzi yake yasiyoisha kwa mtunzi huyo wa kibao 'Mi Amor.'

Kwenye akaunti yake ya Snapchat, mpenzi huyo wa zamani wa Rayvanny alibainisha hatimaye amepata mpenzi wa ndoto yake.

Paula aliendelea kubainisha kuwa anafurahia sana mahusiano yake na mwimbaji huyo wa nyimbo za bongofleva.

"Nimepata mwanaume ninayemtaka, nina furaha," alichapisha.