Bahati azungumzia Diana Marua alivyoficha maisha yake ya anasa wakianza kuchumbiana, alivyomhubiria

"Sikutaka tukosane ama uone mimi ni msherati," Diana Marua alisema.

Muhtasari

•Diana Marua alifichua kwamba alikuwa mpenda anasa ilhali mumewe Bahati alijihusisha zaidi na masuala ya kanisa.

•Diana alifichua kuwa hakutaka kumkosea Bahati kwa vyovyote vile au kumwacha ajue kuhusu maisha ya anasa.

Diana Marua na mumewe Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwimbaji Kelvin Bahati na mkewe Diana Marua wamezungumza kuhusu mitindo yao ya maisha tofauti kabisa wakati walipokutana miaka sita iliyopita.

Akizungumza kwenye chaneli yake ya YouTube, Diana alifichua kwamba alikuwa mpenda anasa ilhali mumewe alijihusisha zaidi na masuala ya kanisa.

Bahati alifichua kwamba hata angemhubiria mama huyo wa watoto wake watatu baada ya  yeye kutoka kujiburudisha kwenye kilabu.

"Tukipatana nilikuwa namhubiria kumhubiria," Bahati alisema.

Alifichua kwamba alikuwa akimpigia simu Diana mara nyingi na angemdanganya kwamba yuko kwenye supermarket ilhali alikuwa kwenye kilabu akiburudika.

Bahati pia alizungumzia jinsi rapa huyo aliavyokuwa akitafuna chingamu kabla ya kukutana naye ili asijue alikuwa ametoka kunywa pombe.

"Nilikuwa nampigia simu namwambia nataka tuonane. Akikuja nilikuwa naona amelewa lakini ako tu... Alafu anatafuna na kujidhibiti," Bahati alifichua.

Diana alisema, "Nilikuwa nachukua maPK natafuna natafuna. Lakini babe kusema kweli nilikuwa nakuheshimu."

Mwanavlogu huyo alifichua kuwa hakutaka kumkosea Bahati kwa vyovyote vile au kumwacha ajue kuhusu maisha ya anasa.

"Sikutaka tukosane ama uone mimi ni msherati," Diana alisema.

Mama huyo wa watoto watatu pia alimfichulia mumewe sababu kuu kwa nini hakutuka kutulia naye kwenye ndoa mwanzoni.

Alidokeza kuwa alipokutana mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alikuwa mtakatifu sana, jambo ambalo hakuridhishwa nalo.

'Ulikuwa Bible, Bible, Bible, Bible. Nilikuwa nakuheshimu," Diana alisema.

Diana pia alifichua kuwa sababu nyingine kwa nini alikuwa na shaka kuhusu kuolewa na Bahati ni tofauti zao za umri.

Alisema kwamba matarajio  yake ya awali yalikuwa kuolewa na mwanamume ambaye ni mkubwa zaidi yake kiumri.

Diana alibainisha kwamba Bahati kuwa mdogo kwake kwa miaka mitatu kulimfanya aone kana kwamba hawakufaana..

"Sababu kuu ilikuwa umri. Wewe ni mdogo kuliko mimi kwa miaka mitatu. Jamii inaamini kuwa kama mwanamke huwezi kuchumbiana na mtu mdogo kuliko yeye. Ata mimi nilijua nikitaka kutulia nitatulia na mtu ambaye ana umri mkubwa kuniliko. Bora awe mkubwa kuniliko kwa mwaka mmoja tuko sawa,” Diana Marua alimwambia mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili kwenye video hiyo.

Wanandoa hao mashuhuri walikuwa wakizungumza kuhusu safari yao ya mahusiano na jinsi walivyoanza kuchumbiana.

Bahati ndiye aliyemuuliza mkewe kwa nini mwanzoni hakutaka kutulia naye kwenye ndoa.

“Tulipoanza kuchumbiana, mbona ulikuwa unaona kama siwezi kukuoa. Na sasa hivi uko hapa uko na watoto wangu nimekupea mimba moja, mbili, tatu, nne. Kwa nini uliona kama siwezi kukuoa,” Bahati alimuuliza mkewe.