Mwimbaji Chameleone atolewa hospitalini kwa wheelchair, atoa taarifa kuhusu afya yake

Pia alionyesha imani yake kwamba hivi karibuni atapata afya yake nzuri.

Muhtasari

•Chameleone aliwashukuru mashabiki wake, marafiki na familia yake kwa kusimama naye katika kipindi ambacho alikuwa hospitalini.

•Chameleone aliambatanisha taarifa yake na video iliyomuonyesha akihamishwa kutoka hospitali kwa kiti cha magurudumu.

Image: INSTAGRAM// CHAMELEONE

Mwimbaji mkongwe wa Uganda Jose Chameleone hatimaye ameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kulazwa kwa siku chache katika Hospitali ya Aline Medical katika jimbo la Minnepolis, Marekani.

Habari kuhusu kulazwa kwake hospitalini ziliibuka siku chache zilizopita huku ripoti zikionyesha kuwa alikuwa akiugua maradhi ya tumbo.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili, mwimbaji huyo wa Uganda aliwashukuru mashabiki wake, marafiki na familia yake kwa kusimama naye katika kipindi ambacho alikuwa hospitalini.

“Nataka kuchukua muda kueleza shukrani zangu za dhati kwa upendo, usaidizi, na maombi ambayo nilipokea wakati wa kulazwa hospitalini. Maombi yenu mazuri yamenipa nguvu katika wakati huu mgumu,” Chameleon alisema katika taarifa.

Mtunzi huyo wakibao ‘Valu Valu’ pia alitoa shukrani kwa hospitali  ya Marekani ambako alikuwa amelazwa kwa kumhudumia na akabainisha kuwa sasa yuko katika harakati ya kupona kabisa.

Pia alionyesha imani yake kwamba hivi karibuni atapata afya yake nzuri.

“Ijapokuwa kupona kwangu bado kunaweza kuhitaji muda na subira, nina hakika kwamba nitarejea katika afya njema hivi karibuni. Mungu amekuwa mwema kwangu siku zote,” alisema

Chameleone aliambatanisha taarifa yake na video iliyomuonyesha akihamishwa kutoka hospitali kwa kiti cha magurudumu. (wheelchair).

Wiki iliyopita, babake Chameleone aliiambia Bukedde TV kwamba nyota huyo mwenye umri wa miaka 44 amekuwa na matatizo ya tumbo.

“Chameleone amekuwa mgonjwa katika miezi iliyopita. Alipohamia Amerika, ugonjwa ulizidi kuwa mbaya. Sasa ni mgonjwa sana, yuko kwenye kitanda chake cha wagonjwa. Amekuwa akipata matatizo kwenye tumbo ambayo anapatiwa matibabu kwa sasa." babake Chameleone.

Mwimbaji wa Uganda Gravitty Omutujji pia alitoa wito kwa mastaa wenzake wa Uganda kuja pamoja na kumuombea mwimbaji huyo.

“Kama nchi, tunatakiwa kumuombea Chameleone, marafiki zake, na kila mtu popote pale mlipo muombee Chameleone kwa sababu anaumwa sana. Wakati huo nilipompigia simu, alikuwa anaelekea kwenye chumba cha AU kwa ajili ya upasuaji,” Gravitty alisema.

Mwaka wa 2021, aliripotiwa kuwa mgonjwa mahututi na yuko ICU. Picha zake akiwa kitandani hospitali akihudumiwa na mama yake Prossy Mayanja zilisambaa.

Msaidizi wake wakati huo, alithibitisha kwa baadhi ya vyombo vya habari vya Uganda kwamba mtunzi huyo wa 'Valu Valu' alikuwa mgonjwa na amelazwa katika Hospitali ya Nakasero.