"Tuko poa sana!" Kajala amsifia mkwewe Marioo huku akiweka wazi uhusiano wao mzuri

“Nafurahi kwamba kanikabidhi mtoto, sio rasmi lakini. Nimefurahi, nashukuru nampenda sana mama yangu," Marioo alisema.

Muhtasari

•Marioo alitumia karamu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Kajala kummiminia upendo mama mkwe huyo wake na kumthamini kwa kumpa binti yake.

•Kabla ya kupokea pesa hizo, Kajala alifunguka kuhusu uhusiano mzuri kati yake na mkwe wake Marioo.

Marioo amkumbatia Kajala mnamo siku yake ya kuzaliwa.
Image: HISANI

Muigizaji mkongwe wa filamu bongo Fridah Kajala Masanja alifanya tafrija kubwa ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumamosi jioni.

Familia, marafiki na wasanii wengine katika tasnia ya bongo walikuwa miongoni mwa wageni waliopamba hafla hiyo huku mama huyo wa binti mmoja akisherehekea kutimiza miaka 40.

Mwimbaji Omary Mwanga almaarufu Marioo, ambaye kwa sasa anachumbiana na bintiye Kajala mwenye umri wa miaka 21, Paula Paul alikuwa miongoni mwa wageni waliopamba sherehe hiyo. Mwimbaji huyo wa kibao ‘Mi Amor’ alitumia hafla hiyo kummiminia upendo mama mkwe wake na kumthamini kwa kumpa binti yake.

“Upendo ambao naupata kutoka kwa mama mkwe ni mkubwa sana. Tushaongea vitu vingi mimi na mama yangu, tumeshapanga vitu vingi sana. Mimi niseme tu nampenda sana na Mungu amfanyie upesi mambo yazidi kuwa mazuri,” Marioo alisema mbele ya wageni waliokuwa wamejumuika kwa karamu hiyo.

Aliongeza, “Nafurahi kwamba kanikabidhi mtoto, sio rasmi lakini. Nimefurahi, nashukuru nampenda sana mama yangu. Mungu akubariki.”

Baada ya hotuba yake, Marioo alifikia begi lililojaa pesa ambazo alikusudia kumpa mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang Harmonize kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Kabla ya kupokea pesa hizo, Kajala alifunguka kuhusu uhusiano mzuri kati yake na mkwe wake Marioo.

Alimtambua mwimbaji huyo kama mwanawe na akafichua kuwa wanafanya mipango mikubwa pamoja.

“Omari ni kijana wangu. Tuko poa sana, tunaingia vizuri mno. Tunaongea vitu vingi sana, ata asiponipa mimi chochote hapa, niko poa kwa sababu kuna vitu vingi sana tunafanya nyuma ya pazia nyinyi hata hamjui. Uwepo wake hapa ni mkubwa mnachotaka atoe kwenye sahani. Shukran kwa kuja,” Kajala alisema.

Baada ya kusifiwa, Marioo aliendelea kumuogesha mama huyo wa mpenzi wake noti za pesa kiasi ambacho hakikujulikana.

Marioo na Paula walifichua kuwa wanachumbiana mapema mwaka huu na wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi wa wazi kwa miezi kadhaa sasa.

Paula alimtambulisha Marioo kama mpenzi wake mpya takriban miezi mitatu iliyopita, siku chache tu baada ya aliyekuwa mpenziwe, Rayvanny kuthibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na mzazi mwenzake Fahyma almaarufu Fayvanny.