Kajala amshabulia vibaya babake Paula mnamo siku ya kina baba, "Hastahili chochote!"

Kajala na P-Funk wamekuwa na uhusiano mbaya na wamesikika mara nyingi wakitupiana maneno mazito hadharani.

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alidokeza kuwa wanaume wanapaswa kuwa na manufaa kwa ili kustahili kutambuliwa.

•Hivi majuzi, Paula aliweka wazi kwamba huwa haoni shida wakati mamake anapomzungumzia vibaya baba yake P-Funk Majani.

Kajala, P-Funk Majani na binti yao Paula
Image: HISANI

Siku ya Jumapili, Juni 18, ulimwengu mzima uliadhimisha siku ya kimataifa ya akina baba.

Mamilioni ya walimwenguni kutoka mataifa mbalimbali waliwasherehekea akina baba muhimu katika maisha yao kwa njia tofauti.  Baadhi waliwapa kina baba zawadi maalum, wengine wakawaandikia jumbe nzuri miongoni mwa njia zingine nyingi maalum za kuwatambua wanaume hao maalum.

Lakini si kwa muigizaji mkongwe wa Tanzania, Frida Kajala Masanja, ambaye alitumia siku hiyo kuwashauri wanawake jinsi ya kuwatendea wanaume. Katika ujumbe wake ambao ulionekana kuwa shambulio lisilo la moja kwa moja kwa mwanamume ambaye jina lake hakulitaja, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alidokeza kuwa wanaume wanapaswa kuwa na manufaa kwa ili kustahili kutambuliwa.

"Mwanaume ambaye hakufanyi chochote hastahili chochote kutoka kwako," Kajala alisema katika nukuu.

Ujumbe wa Kajala Masanja mnamo siku ya akina baba ulionekana kuwa shambulio lisilo la moja kwa moja kwa mzazi mwenzake, mtayarishaji  P-funk Majani ambaye amekuwa akivutana naye kwa miaka mingi  sasa. Wawili hao wana binti mmoja pamoja, mwanamitindo Paula Paul mwenye umri wa miaka 20.

Hivi majuzi, Paula aliweka wazi kwamba huwa haoni shida wakati mamake anapomzungumzia vibaya baba yake P-Funk Majani.

Akiongea kwenye reality show yao 'Behind the Gram', mrembo huyo mwenye umri wa miaka 20 alibainisha kuwa babake ambaye ni mtayarishaji wa muziki mkongwe pia amesikika mara kadhaa akimsema vibaya mama yake hadharani.

Alidokeza kuwa ni mara nyingi  ambapo P-Funk amewahi hata kumtusi Kajala Masanja kwenye majukwaa tofauti ya vyombo vya habari.

"Mama alipokuwa anamzunguzia baba, sikuskia chochote. Kwa sababu baba mwenyewe anakaanga anamtuna mama kwenye vyombo vya habari anamuita stupid sijui na nini," Paula alisema kwenye kipindi cha Behind the Gram.

Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Mwezi uliopita, Kajala akiwa kwenye mahojiano na kituo cha redio cha humu nchini alifichua mahusiano yake na P-Funk yalianza baada ya mtayarishaji huyo kuwahonga wasanii waliokuwa na ukaribu naye ili wampeleke kwake.

"Tulikutana mitaani tu. Mimi nilikuwa mdogo bado nasoma alafu tukakutana.  Aliniona alafu akatuma watu wanitafute," alisimulia.

"Nilikuwa na ukaribu na wasanii kadhaa, aliwaambia wanitafute akiahidi kuwatayarishia albamu mzima bure. Basi wakanipeleka, walinidanganya kwanza tunakoenda. Rich One aliniamba tunaenda kuonana na mtu. Hawakuwa hata na magari tulipanda daladala. Tulienda kwa nyumba tukaoga tumesubiri tukaambiwa huyo mtu ametoka. Baadaye akarudi nikaona mtu nilikutana naye alafu nikampuuza. Nikamuuliza Rich One mbona hakuniambia anakonileta. Basi tukaanza kuongea hadi akatokea Paula," 

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alibainisha kwamba hakuwahi kuwa kwenye ndoa na mtayarishaji huyo wa muziki bali walikuwa tu wapenzi ambao waliishi pamoja kwa muda kisha wakapata mtoto pamoja.

Alisema kwamba mahusiano yao hayakuwahi kufikia kuwa ndoa rasmi kwani wote hawakuwa wamekomaa wakati huo.

"Kipindi hicho nilikuwa bado mdogo. Ata yeye alikuwa na akili za kitoto bado. Kwa hiyo wote tulikuwa wadogo," alisema.

Kajala alisema hali ya kutoelewana kati yao ilipelekea mahusiano yao ya muda kuvunjika na wakaenda njia tofauti.

"Tulishindwana tu. Nashukuru ameniachia Paula. Tuko sawa Tunashirikiana katika malezi," alisema Kajala.

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize hata hivyo alifichua kuwa yeye na mzazi huyo mwenzake huwa hawawasiliana mara kwa mara. Alisema kwa kawaida Paula ndiye huzungumza na babake wakati haja inapotokea.