Paula aeleza kwa nini hana shida wazazi wake Kajala na P-Funk wanapotupiana matusi hadharani

Paula pia alimtaka mamake kumuacha aishi maisha yake atakavyo akidokeza kwamba yeye ni mtu mzima.

Muhtasari

•Paula alibainisha kuwa baba yake  pia amesikika mara kadhaa akimsema vibaya mama yake hadharani.

•Paula pia alilalamika kuhusu mama yake kufuatilia maisha yake sana.

Kajala, P-Funk Majani na binti yao Paula
Image: HISANI

Mwanamitindo wa Tanzania Paula Kajala ameweka wazi kuwa haoni shida mama yake Kajala Masanja anapomzungumzia vibaya baba yake P-Funk Majani.

Akiongea kwenye reality show yao 'Behind the Gram', mrembo huyo mwenye umri wa miaka 20 alibainisha kuwa baba yake ambaye ni mtayarishaji wa muziki mkongwe pia amesikika mara kadhaa akimsema vibaya mama yake hadharani.

Alidokeza kuwa ni mara nyingi  ambapo P-Funk amewahi hata kumtusi Kajala Masanja kwenye majukwaa tofauti ya vyombo vya habari.

"Mama alipokuwa anamzunguzia baba, sikuskia chochote. Kwa sababu baba mwenyewe anakaanga anamtuna mama kwenye vyombo vya habari anamuita stupid sijui na nini," Paula alisema kwenye kipindi cha Behind the Gram.

Katika kipindi hicho, mwanamitindo huyo ambaye anaaminika kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwimbaji Omary Mwanga almaarufu Marioo alilalamika kuhusu mama yake kufuatilia maisha yake sana.

Kufuatia hayo, Paula alimtaka mama yake kumuacha aishi maisha yake atakavyo akidokeza kwamba sasa yeye ni mtu mzima. 

"Yaani anafaa kuniacha niishi maisha yangu, mimi ni msichana mkubwa sana," Paula alisema.

Mwezi uliopita, Kajala akiwa kwenye mahojiano na kituo cha redio cha humu nchini alifichua mahusiano yake na P-Funk yalianza baada ya mtayarishaji huyo kuwahonga wasanii waliokuwa na ukaribu naye ili wampeleke kwake.

"Tulikutana mitaani tu. Mimi nilikuwa mdogo bado nasoma alafu tukakutana.  Aliniona alafu akatuma watu wanitafute," alisimulia.

"Nilikuwa na ukaribu na wasanii kadhaa, aliwaambia wanitafute akiahidi kuwatayarishia albamu mzima bure. Basi wakanipeleka, walinidanganya kwanza tunakoenda. Rich One aliniamba tunaenda kuonana na mtu. Hawakuwa hata na magari tulipanda daladala. Tulienda kwa nyumba tukaoga tumesubiri tukaambiwa huyo mtu ametoka. Baadaye akarudi nikaona mtu nilikutana naye alafu nikampuuza. Nikamuuliza Rich One mbona hakuniambia anakonileta. Basi tukaanza kuongea hadi akatokea Paula," 

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alibainisha kwamba hakuwahi kuwa kwenye ndoa na mtayarishaji huyo wa muziki bali walikuwa tu wapenzi ambao waliishi pamoja kwa muda kisha wakapata mtoto pamoja.

Alisema kwamba mahusiano yao hayakuwahi kufikia kuwa ndoa rasmi kwani wote hawakuwa wamekomaa wakati huo.

"Kipindi hicho nilikuwa bado mdogo. Ata yeye alikuwa na akili za kitoto bado. Kwa hiyo wote tulikuwa wadogo," alisema.

Kajala alisema hali ya kutoelewana kati yao ilipelekea mahusiano yao ya muda kuvunjika na wakaenda njia tofauti.

"Tulishindwana tu. Nashukuru ameniachia Paula. Tuko sawa Tunashirikiana katika malezi," alisema Kajala.

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize hata hivyo alifichua kuwa yeye na mzazi huyo mwenzake huwa hawawasiliana mara kwa mara. Alisema kwa kawaida Paula ndiye huzungumza na babake wakati haja inapotokea.