Kajala afunguka alivyotongozwa na babake Paula akiwa mdogo, kwa nini mahusiano hayakudumu

"Kipindi hicho nilikuwa bado mdogo. Ata yeye alikuwa na akili za kitoto bado," alisema

Muhtasari

• Kajala alifichua mahusiano yao yalianza baada ya mtayarishaji huyo wa muziki kuwahonga wasanii waliokuwa na ukaribu naye ili wampeleke kwake.

•Alisema hakuwahi kuwa kwenye ndoa naP-Funk  bali walikuwa wapenzi ambao waliishi pamoja kwa muda kisha wakapata mtoto pamoja.

•Kajala alidai kwa sasa anachumbiana na mwanasiasa wa Kenya ambaye anatazamani kupata mtoto naye

Kajala, P-Funk Majani na binti yao Paula
Image: HISANI

Muigizaji maarufu wa filamu bongo, Frida Kajala Masanja amefunguka kuhusu mahusiano yake yaliyosambaratika na mtayarishaji P-Funk Majani.

Kajala na Majani walichumbiana takriban miongo miwili iliyopita na wakajaliwa mtoto mmoja wa kike mrembo pamoja, Paula Paul Kajala.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Kajala alifichua mahusiano yao yalianza baada ya mtayarishaji huyo wa muziki kuwahonga wasanii waliokuwa na ukaribu naye ili wampeleke kwake.

"Tulikutana mitaani tu. Mimi nilikuwa mdogo bado nasoma alafu tukakutana.  Aliniona alafu akatuma watu wanitafute," alisimulia.

"Nilikuwa na ukaribu na wasanii kadhaa, aliwaambia wanitafute akiahidi kuwatayarishia albamu mzima bure. Basi wakanipeleka, walinidanganya kwanza tunakoenda. Rich One aliniamba tunaenda kuonana na mtu. Hawakuwa hata na magari tulipanda daladala. Tulienda kwa nyumba tukaoga tumesubiri tukaambiwa huyo mtu ametoka. Baadaye akarudi nikaona mtu nilikutana naye alafu nikampuuza. Nikamuuliza Rich One mbona hakuniambia anakonileta. Basi tukaanza kuongea hadi akatokea Paula," 

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alibainisha kwamba hakuwahi kuwa kwenye ndoa na mtayarishaji huyo wa muziki bali walikuwa tu wapenzi ambao waliishi pamoja kwa muda kisha wakapata mtoto pamoja.

Alisema kwamba mahusiano yao hayakuwahi kufikia kuwa ndoa rasmi kwani wote hawakuwa wamekomaa wakati huo.

"Kipindi hicho nilikuwa bado mdogo. Ata yeye alikuwa na akili za kitoto bado. Kwa hiyo wote tulikuwa wadogo," alisema.

Kajala alisema hali ya kutoelewana kati yao ilipelekea mahusiano yao ya muda kuvunjika na wakaenda njia tofauti.

"Tulishindwana tu. Nashukuru ameniachia Paula. Tuko sawa Tunashirikiana katika malezi," alisema Kajala.

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize hata hivyo alifichua kuwa yeye na mzazi huyo mwenzake huwa hawawasiliana mara kwa mara. Alisema kwa kawaida Paula ndiye huzungumza na babake wakati haja inapotokea.

Hata hivyo, alifichua kwamba ana uhusiano mzuri sana na mke wa sasa wa P-Funk na huwa wanazungumza sana.

"Mke wake mshikaji wangu. Tunaongea sana. Sisi ni marafiki kabisa. Yeye ni wa kupiga stori na kuchat. Naweza kuwa sijaongea na P kwa miezi kadhaa ama miaka lakini mke wake tunaongea naye," Kajala alisema.

Kajala alidai kwa sasa anachumbiana na mwanasiasa wa Kenya ambaye anatazamani kupata mtoto naye. P-Funk kwa upande wake amekuwa kwenye ndoa na mwanamke mwingine kwa zaidi ya muongo mmoja na wana watoto pamoja.