Kajala akiri kusherehekea Paula na Rayvanny walipoachana, afichua kwa nini hakuidhinisha mahusiano yao

Kajala amefichua hakufurahi wakati alipogundua binti yake Paula yupo kwenye mahusiano na Rayvanny.

Muhtasari

•Kajala aliweka wazi kuwa pia yeye alikuja kufahamu kuhusu mahusiano hayo kupitia mitandao ya kijamii.

•Kajala alisema alijaribu kumshauri Paula dhidi ya mahusiano na Rayvanny lakini juhudi zake  ziliangukia patupu kwani Paula hakusikia.

Rayvanny, Paula, Kajala
Image: HISANI

Muigizaji wa filamu bongo Frida Kajala Masanja amefichua kuwa hakufurahi wakati alipogundua binti yake Paula Paul yupo kwenye mahusiano na mwanamuziki Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny takriban miaka miwili iliyopita.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha humu nchini, Kajala aliweka wazi kuwa pia yeye alikuja kufahamu kuhusu mahusiano hayo kupitia mitandao ya kijamii kama wanamitandao wengine wote.

"Paula hata hakuwa na nguvu za kuniambia. Ilitokea tukaona huko mitandaoni. Alikuwa 18. Kwa mawazo yangu nilijua Paula hana mpenzi," alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alibainisha kwamba kwa kweli bintiye alichumbiana na Rayvanny kabla ya kutengana. Licha ya kutopendezwa na mahusiano yao, aliweka wazi kuwa hakuhusika katika kutengana kwao.

Hata hivyo alikiri kwamba alijaribu sana kumshauri mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 dhidi ya mahusiano na bosi huyo wa Next Level Music lakini juhudi zake  ziliangukia patupu kwani Paula hakusikia.

"Nilijaribu sana kumweleza kwamba hii sio sahihi lakini mtu anaenda anafanya kinyume, inabidi umeacha tu. Ukimwambia asiende na huyo mtu anasema sawa lakini bado anaendelea. Nilijaribu kumzuia sana," alisema.

Aidha, alisema baada ya kushindwa kumshauri Paula dhidi ya uhusiano huo, alimshauri jinsi ya kujiendeleza katika mahusiano.

"Nilimwambia kwa sababu yeye bado ni mdogo atulie bado ana maisha mbele. Asifanye vitu kwa hasira," alisema.

Kajala alisema alifurahi wakati mahusiano ya bintiye na Rayvanny yaligonga mwamba kwa sababu hakuona ndoa pale.

"Nilifurahi kwa sababu nahisi hapo hakuna future pale. Paula mdogo, Ray tayari ana mwanamke wake na amezaa naye. Sidhani kwamba angeacha familia yake kwa sababu ya Paula, sijui labda angerudi kwa mwanamke wake," alisema.

Muigizaji huyo alithibitisha kwamba binti yake bado hajatimiza umri wa kujisimamia kabisa na akafichua bado anaishi naye.

Alipoulizwa ikiwa kwa kweli Paula anachumbiana na msanii mwingine wa Bongo, Omary Mwanga almaarufu Marioo, alisema "Kwa kweli sijui. Yeye ananiambia hayupo kwenye mahusiano lakini picha tunaziona.

Rayvanny na Paula wanaaminika kuchumbiana 2021 kabla ya kutengana katika hali tatanishi. Harmonize alidaiwa kujaribu bahati yake kwa mwanamitindo huyo wakati akichumbiana na mama yake, Kajala Masanja.