Kajala afunguka uhusiano na Harmonize baada ya kuachana, kumtambulisha mpenzi wake mpya

"Hiyo imepita miezi mingi sana. Hatuna haja ya kuizungumzia." alisema.

Muhtasari

•Kajala alisema alifurahi sana alipoitwa kwa ajili ya hafla ya hisani ya Nazarene Ophans Center itakayofanyika katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.

•Kajala pia aliweka wazi kwamba mwanamuziki Mista Champagne ambaye alimuimbia wimbo mzuri hivi karibuni ni rafiki yake tu.

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Kajala
Image: HISANI

Muigizaji maarufu wa filamu Bongo, Frida Kajala Masanja yupo nchini Kenya kwa ajili ya Hafla ya Hisani itakayofanyika siku ya Jumamosi.

Akizungumza na wanahabari baada ya kutua nchini Kenya Ijumaa asubuhi, Kajala alisema alifurahi sana alipoitwa kwa ajili ya hafla ya hisani ya Nazarene Ophans Center itakayofanyika katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.

"Nilifurahi. Ndio maana nimekuja na nitashiriki kwa namna moja ama nyingine," alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo, Harmonize alithibitisha atakutana na mashabiki wake Wakenya wakati wa ziara yake.

Kando na kuzungumzia  kilichomleta Kenya, Kajala alishinikizwa kujibu swali kuhusu hali yake ya mahusiano.

Alipotakiwa kuzungumza kuhusu uhusiano wake wa sasa na bosi wa Kondegang, alisema, "Hiyo hatuwezi kuongelea hapa. Tumekuja kuongelea hisani. Hiyo imepita miezi mingi sana. Hatuna haja ya kuizungumzia."

Mama huyo wa binti mmoja pia aliombwa kujibu kuhusu ikiwa anapanga kutambulisha mpenzi mpya hivi karibuni. Alijibu, "Hapana."

Kajala pia aliweka wazi kwamba mwanamuziki Mista Champagne ambaye alimuimbia wimbo mzuri hivi karibuni ni rafiki yake tu.

"Wimbo wake ni mzuri sana. Ameniniimbia, naipenda. Champagne ni rafiki yangu mzuri. Tumekuwa marafiki.Tuko sawa," alisema.

Mapema mwezi huu, Harmonize alikiri kwamba Kajala Masanja alimfanya kuandika wimbo wake wa  'Single Again.'

Bosi huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alifichua kwamba alifanya wimbo huo ambao umeendelea kutamba sana kama njia ya kuponya jeraha la moyo alilopata baada ya kutengana na muigizaji huyo.

"Nilikuwa katika mapenzi. Nilikuwa nikitafuta njia nzuri ya kupona kufuatia utengano wenye maumivu. Niliishia kutengeneza wimbo huu wa kimataifa," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Hata hivyo, aliweka wazi kwamba sasa anaendelea vizuri, takriban miezi mitatu baada ya mahusiano hayo kugonga mwamba.

Mwimbaji huyo alitengana na muigizaji Frida Kajala Masanja mapema mwezi Desemba baada ya kuchumbiana kwa miezi kadhaa. Takriban miezi miwili baadaye, Konde Boy aliachia 'Single Again' kubainisha hali yake ya mahusiano ya sasa. 

Wakati akitangaza kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.