Kajala avunja kimya baada ya Harmonize kutumia vixen anayefanana naye kwenye 'Single Again'

Muigizaji huyo alimtema Harmonize Desemba mwaka jana baada ya kuchumbiana takriban miezi 7.

Muhtasari

•Harmonize alitumia video vixen anayefanana sana na aliyekuwa mpenziwe, Kajala kwenye video ya wimbo 'Single Again'.

•Muigizaji huyo alionekana kudokeza kuwa Konde Boy anamuonea gere kwa maendeleo yake baada ya kutengana mwaka jana.

Kajala, Caren Simba na Harmonize
Image: HISANI

Hatimaye staa wa Bongo Harmonize aliachia video ya wimbo wake unaovuma 'Single Again' ambayo ilikuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alichapisha video ya kuvutia ya kwenye chaneli yake ya mtandao wa Youtube siku ya Jumatatu jioni.

Kilichojitokeza zaidi kwenye video ya wimbo huo ni kwamba alimtumia video vixen anayefanana sana na aliyekuwa mpenziwe, Kajala Masanja.

"Shukran Caren Simba," Harmonize alimshukuru vixen huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne.

Vixen huyo alifanana na muigizaji huyo mkongwe kuanzia kwa mwonekano wa mwili, mtindo wa nywele hadi kwenye uvaaji.

Kwa kweli, kama vile wengi wetu tuliotazama video hiyo tuligundua alichofanya mwimbaji huyo, Kajala naye pia aliona na kujibu.

"Hapa duniani kuna watu wanapenda kujitekenya alafu wanacheka wenyewe saa ndio nini," Kajala aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram baadaye siku ya Jumanne na kuambatanisha na emoji ya kicheko.

Ujumbe wa mama huyo wa binti mmoja ulionekana kuwa jibu la wazi kwa mpenzi huyo wake wa zamani kufuatia alichokifanya.

Muigizaji huyo pia alionekana kudokeza kuwa Konde Boy anamuonea gere kwa maendeleo yake baada ya kutengana mwaka jana.

"Watu wanaweza kuwa na zaidi yako na bado wakawa na wivu," alisema kwa kutumia meme.

Harmonize aliachia wimbo 'Single Again' mnamo siku ya wapendanao, takriban miezi miwili baada ya mahusiano yao kuvunjika.

Wawili hao walitengana Desemba mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa takriban miezi saba. Walikuwa wamerudiana mwezi Aprili baada ya Harmonize kunyenyekea na kumuomba radhi muigizaji huyo kwa makosa aliyomtendea awali.

Wakati akitangaza kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.