"Mapenzi yalinitesa!" Kajala akiri huku akifurahia upweke miezi baada ya kumtema Harmonize

Kajala alidokeza kwamba alipitia masaibu mengi wakati wa mahusiano yake na Harmonize.

Muhtasari

•Muigizaji mkongwe Frida Kajala Masanja anaonekana kuendelea vizuri na hali yake mpya ya mahusiano.

•Wiki chache zilizopita, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alidokeza kwamba yupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mapya.

Harmonize na Kajala
Image: HISANI

Muigizaji mkongwe Frida Kajala Masanja anaonekana kuendelea vizuri na hali yake mpya ya mahusiano, ikiwa ni miezi michache tu baada ya kutengana na bosi wa Kondegang Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize.

Wasanii ha walitengana Disemba mwaka jana na Kajala sasa ameonekana kutupa vijembe kwa mahusiano hayo ya miezi michache.

Siku ya Jumatano, mama huyo wa binti mmoja, kwa njia isiyo ya moja kwa moja alidokeza kuwa alipitia masaibu mengi katika mahusiano hayo. Alifanya hivyo kwa kuchapisha video yake akicheza na kuimba wimbo mpya wa Alikiba 'Mahaba' ambao unazungumzia masaibu yanayohusiana na mahusiano sumu.

"Uchungu wa kulia daily

Mapenzi yalinifanya nisile

Sina kumbukumbu ile

Kwamba ulinitosha, no

Mwenzako mi nilikufa, nikaziwa, nikaoza

Mapenzi yalinitesa, yalinitupa, nimefufuka yeah

Mi nilikufa, nikaziwa, nikaoza

Mapenzi yalinitesa, nimefufuka yeah," aliimba.

Wiki chache zilizopita, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alidokeza kwamba yupo tayari kujitosa kwenye mahusiano mapya.

Mama huyo wa binti mmoja aliweka wazi kwamba sasa yuko tayari kujaribu mahusiano na mtu wa ishara sawa ya zodiac na yeye, kumaanisha mtu anayesherehekea siku ya kuzaliwa karibu wakati sawa wa mwaka naye.

"Nataka kuchumbiana na ishara yangu. Nataka nione kama tutakuwa na tabia sawa na kama tutadumu," alisema kwenye Instagram.

Wakati akitangaza kutengana na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana, Kajala aliweka wazi kwamba alikuwa tayari kupiga hatua nyingine baada ya mahusiano yao ya miezi michache kugonga mwamba.

Ingawa hakufichua kilichowatenganisha, aliweka wazi kwamba hakubeba kinyongo chochote dhidi ya mwimbaji huyo.

"Mimi kama mwanamke na binadamu nimeumbwa kupenda na kusamehe pia, ila kwenye hili nastahili kuchekwa, nastahili kubezwa na kudharauliwa pia. Sipo hapa kujitetea wala kutia huruma ni kweli nilifanya makosa na nimeyagundua makosa yangu, mimi siyo mkamilifu," Kajala alisema mwezi Desemba.

Wapenzi hao wa zamani walikuwa wamechumbiana kwa takriban miezi saba kabla ya kwenda njia tofauti mapema mwezi Desemba. Wawili hao walikuwa wamerudiana Aprili baada ya Harmonize kuomba msamaha.

Wakati wa mahusiano yao, wawili hao walionekana kuwa na muungano mzuri na kufurahia kuwa pamoja. Mwezi Juni walidokeza mpango wa kufunga pingu za maisha huku Harmonize akimvisha Kajala pete ya uchumba.