Zuchu afichua sababu halisi ya kutengana na Diamond, aibua malalamiko mazito dhidi yake

Malkia huyo wa bongo amelalamika kwamba Diamond amemuweka katika hatari ya kushambuliwa na kukosewa heshima.

Muhtasari

•Zuchu hatimaye amejitokeza kuweka mambo wazi kuhusu kwa nini aliondoka kwenye mahusiano yake na Diamond Platnumz.

•Alilalamika kwamba kila jambo linapotokea linalohusisha watu katika maisha ya Diamond, kila mara lengo linaelekezwa kwake.

Zuchu amezungumzia sababu ya kumtema Diamond

Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu hatimaye amejitokeza kuweka mambo wazi kuhusu kwa nini aliondoka kwenye mahusiano yake na Diamond Platnumz.

Kwa muda mrefu mastaa hao wawili wa bongo fleva wanaoonekana kuwa na ushirikiano mzuri wa kimuziki wamekuwa wakiaminika kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi ambao umekuwa na misukosuko mingi. Hata hivyo, hivi majuzi Zuchu aliripotiwa kuvunja uhusiano huo, huku tetesi nyingi zikizunguka hali hiyo.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, binti huyo wa malkia wa taarab Khadija Kopa hata hivyo alieleza kuwa Diamond amemfanya ashambuliwe kwa urahisi kupitia maisha yake yenye utata Alimshutumu mpenzi huyo wake kwa kumweka kwenye hatari ya kutoheshimiwa na watu, jambo ambalo sasa amechoka nalo.

“I know mimi ni maarufu na kuongelewa ni kawaida. But kindly msipitilze kunipa sifa za uongo mradi kumpamba boss haswa kwa media ya nyumbani ambayo mnaweza pia kupata ukweli wa mambo mkasawazisha stori zenu,” Zuchu alilalamika kwenye ukurasa wake wa Instagram.  

Aliendelea, “Hii ndio sababu hasa kwa nini niliondoka, unachoka kuwa na mwanaume anayekusukuma kwa watu utukanwe na yeye ndo anayetumika kwenye kudhalilika kwako. Mwanamke wake ndo kanyagio la kila aliyemzunguka , akiamua tu basi yeye huungana nao na kuwapa vichwa vya kunivunjishia heshima ilhali umekaa kimya na unachofanya tu ni kukaa na kumeza. Ninajaribu kuwa mtu mzuri na kiungo dhaifu katika maisha yangu ni yeye."

Mwimbaji huyo mrembo alitoa wito kwa watu kuwa rahisi kwake na kumruhusu kuwa na amani.

Alilalamika kwamba kila jambo linapotokea linalohusisha watu katika maisha ya Diamond wakiwemo wazazi wenzake na wapenzi wake wa zamani, kila mara lengo linaelekezwa kwake.

“Hamkai kusema sababu yeye, anayesababisha mtu unataka kuondoka zake. Baby mama wakiamka na hasira waje na wao wanakutupia attitude zao kwa Zuchu. Maex nisiowajua content yao wanapewa wakusema ni Zuchu. Maadui zangu ashirikiane nao wakikaa na huyo mwanaume anawapa nguvu ni Zuchu,” aliandika.

Kauli ya Zuchu inakuja wakati anaripotiwa kuachana na Diamond.

Kulikuwa na tetesi kuwa aliondoka baada ya bosi huyo wa WCB kumtambulisha ex wake Sarah jukwaani wakati wa tamasha lililofanyika hivi majuzi nchini Tanzania.