Harmonize adhihaki mahusiano yake na Kajala yaliyovunjika, ashauri watu kuwa makini na mapenzi

Mwimbaji huyo ameshauri watu kuwa makini wakati linapokuja suala la mahusiano.

Muhtasari

•Harmonize alitumia matatizo yake ya kimapenzi kama mfano wa jinsi mahusiano yanavyoweza kubadilika kutoka kuwa mazuri hadi mabaya.

•Harmonize alitengana na muigizaji Frida Kajala Masanja mapema mwezi Desemba baada ya kuchumbiana kwa miezi kadhaa.

Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake Kajala
Image: HISANI

Bosi wa lebo ya Konde Music Worldwide almaarufu Harmonize ametoa ushauri kwa watu kuwa makini wakati linapokuja suala la mahusiano.

Harmonize alitumia matatizo yake ya kimapenzi kama mfano wa jinsi mahusiano yanavyoweza kubadilika kutoka kuwa mazuri hadi mabaya.

Alibainisha kuwa aliwahi kusema mapenzi yake na Kajala ni hadi kifo na sasa anaimba kwamba yuko single tena.

"Kuweni makini na mapenzi. Huyu huyu aliyeimba tuzikwe wote ndio anayeimba I'm single again," alisema kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo alitengana na muigizaji Frida Kajala Masanja mapema mwezi Desemba baada ya kuchumbiana kwa miezi kadhaa.

Takriban miezi miwili baadaye, Konde Boy aliachia wimbo 'Single Again' kubainisha hali yake ya mahusiano ya sasa. Tangu kuachia wimbo huo mnamo siku ya wapendanao, mwanamuziki huyo amekuwa akiupigia debe kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na aliachia video rasmi mapema wiki hii.

Staa huyo wa muziki wa Bongo alichapisha video ya kuvutia ya kwenye chaneli yake ya mtandao wa Youtube siku ya Jumatatu jioni.

Kilichojitokeza zaidi kwenye video ya wimbo huo ni kwamba alimtumia video vixen anayefanana sana na aliyekuwa mpenziwe, Kajala Masanja.

"Shukran Caren Simba," Harmonize alimshukuru vixen huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne.

Vixen huyo alifanana na muigizaji huyo mkongwe kuanzia kwa mwonekano wa mwili, mtindo wa nywele hadi kwenye uvaaji.

Kwa kweli, kama vile wengi wetu tuliotazama video hiyo tuligundua alichofanya mwimbaji huyo, Kajala naye pia aliona na kujibu.

"Hapa duniani kuna watu wanapenda kujitekenya alafu wanacheka wenyewe saa ndio nini," Kajala aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram baadaye siku ya Jumanne na kuambatanisha na emoji ya kicheko.

Ujumbe wa mama huyo wa binti mmoja ulionekana kuwa jibu la wazi kwa mpenzi huyo wake wa zamani kufuatia alichokifanya.

Muigizaji huyo pia alionekana kudokeza kuwa Konde Boy anamuonea gere kwa maendeleo yake baada ya kutengana mwaka jana.

"Watu wanaweza kuwa na zaidi yako na bado wakawa na wivu," alisema kwa kutumia meme.