"Nilikuwa katika mapenzi" Harmonize afunguka kuhusu kuvunjwa moyo na Kajala

Alikiri aliimba 'Single Again' ili kuponya jeraha la moyo alilopata baada ya kutengana na muigizaji huyo.

Muhtasari

•Harmonize amekiri kwamba aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja alimfanya kuandika wimbo wake wa mwezi jana 'Single Again.'

•Harmonize aliweka wazi kwamba sasa anaendelea vizuri, takriban miezi mitatu baada ya mahusiano hayo kugonga mwamba.

Kajala na Harmonize wakati mahaba yao yalikuwa yamenoga
Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amekiri kwamba aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Frida Kajala Masanja alimfanya kuandika wimbo wake wa mwezi jana 'Single Again.'

Akizungumza siku ya Jumapili, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alifichua kwamba alifanya wimbo huo ambao umeendelea kutamba kama njia ya kuponya jeraha la moyo alilopata baada ya kutengana na muigizaji huyo.

"Nilikuwa katika mapenzi. Nilikuwa nikitafuta njia nzuri ya kupona kufuatia utengano wenye maumivu. Niliishia kutengeneza wimbo huu wa kimataifa," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Hata hivyo, aliweka wazi kwamba sasa anaendelea vizuri, takriban miezi mitatu baada ya mahusiano hayo kugonga mwamba.

Wakati huohuo, aliweka wazi kwamba anapendelea kutengeneza nyimbo kutokana na mambo ambayo anapitia maishani.

"Kama tulikuwa na muda pamoja, tarajia kuona chochote ulichonitendea. Kwa hivyo, hakikisha unanitendea mema. Ukinitendea ubaya, nitaendelea kujivunia wewe," alisema.

Mwimbaji huyo wa Bongo alifichua kuwa wazo la kutumia vixen anayefanana na Kajala lilikuwa la mwelekezaji wake Director Kenny.

"Kenny alisema kila mtu anajua kuwa ninapenda makalio makubwa kwa hivyo tupate msichana mwenye makalio makubwa. Hatimaye tukatengeneza wimbo wa dunia," alisema bosi huyo wa Konde Music Worldwide.

"Wakati mwingine ni vizuri kuvunjika moyo. Kaa single, ni ngumu sana kusonga mbele"

Harmonize aliachia video ya kuvutia ya  wimbo 'Single Again' kwenye chaneli yake ya mtandao wa Youtube mapema wiki iliyopita.

Kilichojitokeza zaidi kwenye video ya wimbo huo ni kwamba alimtumia video vixen anayefanana sana na aliyekuwa mpenziwe, Kajala Masanja.

"Shukran Caren Simba," Harmonize alimshukuru vixen huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne.

Vixen huyo alifanana na muigizaji huyo mkongwe kuanzia kwa mwonekano wa mwili, mtindo wa nywele hadi kwenye uvaaji.

Kwa kweli, kama vile wengi wetu tuliotazama video hiyo tuligundua alichofanya mwimbaji huyo, Kajala naye pia aliona na kujibu.

"Hapa duniani kuna watu wanapenda kujitekenya alafu wanacheka wenyewe saa ndio nini," Kajala aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram baadaye siku ya Jumanne na kuambatanisha na emoji ya kicheko.

Ujumbe wa mama huyo wa binti mmoja ulionekana kuwa jibu la wazi kwa mpenzi huyo wake wa zamani kufuatia alichokifanya.

Muigizaji huyo pia alionekana kudokeza kuwa Konde Boy anamuonea gere kwa maendeleo yake baada ya kutengana mwaka jana.

"Watu wanaweza kuwa na zaidi yako na bado wakawa na wivu," alisema kwa kutumia meme.

Mwezi Februari, Harmonize alidokeza kuwa mama yake mzazi alimtahadharisha kuhusu aliyekuwa mpenzi wake, Kajala.

Katika ufichuzi ambao alifanya kama ushauri, bosi huyo wa Kondegang aliwashauri watu kuwapa sikio wazazi wao kila siku..

Konde Boy  alibainisha kwamba wazazi huwa na jicho maalum la kuwasaidia kuona mambo yaliyofichwa ndani ya mtu.

"Msikilize mama!! Awe ni mama yako mzazi au mama wa mwenzio, baba yako ama wa mwenzio.. wazazi wanakuwanga na jicho la mbali sana. Mzazi ni rahisi kugundua kila kitu. Inawezekana ukawa unajiona unajua kila kitu kumbe kuna jicho la mama. Akiangalia kitu au mtu anapata jibu sahihi kuliko wewe," alisema siku ya Alhamisi.

Mwimbaji huyo mahiri aliwasihi watu kutilia maanani pingamizi zinazowekwa na wazazi wao bila kujali jinsi zinavyochukiza.

Pia aliwataka watu kuwasikiliza wazazi wa wenzao hasa kuhusu masuala ya uhusiano bila kujali jinsi mahaba yalivyo mazito.

"Unaweza kuona kama kwamba huyu mama hanipendi akiwa mama wa mwenzio kumbe  huenda anajua kwamba mtoto wake hayupo tayari ila anakosa au anashindwa jinsi ya kukufanya uelewe maana upo kwenye dimbwi la mapenzi," alisema.

"Akiwa mzazi wako ni rahisi kukukataza hata kwa kutumia nguvu zote ila ukiwa umezama humuelewi," 

Wakati huo, alifichua kwamba hapo awali karibu aingie kwenye ndoa mbaya ambayo mzazi wake alikuwa amemuonya dhidi yake.

"Mtu anayeitwa mzazi msikilize hata asiyekuwa wako," alisema.