Christina Shusho azungumzia ndoa yake iliyovunjika, awachukulia hatua wanaopotosha

Mwimbaji wa Tanzania Christina Shusho amejitokeza kuzungumzia uvumi kuhusu ndoa yake iliyovunjika.

Muhtasari

•Shusho alibainisha kuwa kumekuwa na maswali mengi yaliyotokana na mahojiano aliyofanya mwaka wa 2020 na 2022.

•Shusho alisema mawakili wake wanafuatilia suala hilo na kufichua kuwa hatua muhimu za kisheria zitachukuliwa.

Christina Shusho
Christina Shusho
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili wa Tanzania Christina Shusho amejitokeza kuzungumzia uvumi kuhusu ndoa yake iliyovunjika.

Katika taarifa yake ya Jumapili jioni, mwimbaji huyo wa kibao ‘Shusha Nyavu’ alibainisha kuwa kumekuwa na maswali mengi yaliyotokana na mahojiano aliyofanya mwaka wa 2020 na 2022.

Hata hivyo alibainisha kuwa atajibu maswali yote kuhusu ndoa yake iliyosambaratika hivi karibuni wakati mwafaka utakapowadia.

“Ndugu zangu, Waziri wa Habari mnaonitafuta na mashabiki kwa ujumla. Ningependa kuchukua nafasi hii kuweka baadhi ya mambo sawa.

Najua mna maswali mengi kutokana na interviews nilizofanya mwaka 2020 na nyingine 2022. Niseme tu maswali haya yote nitayajibu alisema hivi punde na ukweli utajulikana,” Christina Shusho katika taarifa aliyochapisha kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Aidha, mama huyo wa watoto watatu alituma onyo kali kwa blogu na vyombo vya habari akiwaonya dhidi ya kueneza habari za uwongo kuhusiana na ndoa yake.

Shusho alisema mawakili wake wanafuatilia suala hilo na kutangaza kuwa hatua muhimu za kisheria zitachukuliwa.

“Watu wanaotumia jina langu au picha zangu kwenye mitandao ya kijamii kueneza Habari za upotofu na wengine kutukana: Jambo hili lipo kwenye vyombo vya sheria na nina Imani hatua itachukuliwa na mamlaka husika,” alisema.

Aliongeza, “Siku ya kuongea yote nitaongea na naamini ukweli siku zote humuweka mtu uhuru.”

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili aliendelea kuwaomba watu kuwa na subira naye huku baadhi ya taratibu za kisheria zikifuatwa.

"Niwaombe muwe na uvumilivu kipindi hiki ambacho mamlaka husika zinafanya kazi yote yanayoendelea kwa mujibu wa sheria kwa sababu hayupo afanye juu ya sheria ila wote tupo sawa mbele ya macho ya sheria na hakuna haki bila wajibu," alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya ripoti kusambaa kuwa mumewe wa zamani John Shusho alikuwa amezungumza kuhusu maumivu yake baada ya ndoa yao kuvunjika.