Harmonize avunja kimya baada ya ‘Single Again’ kupigwa chini kwenye tuzo za BET 2024

“Unaweza ukatoa wimbo ukafanya vizuri sana, lakini wao wanaangalia vitu tofauti, kwa hiyo ni maamuzi tu. Mimi siwezi kuwa disappointed na tuzo, ni mamuzi ya kitaasisi tu,” alisisitiza.

Muhtasari

• “Unaweza ukatoa wimbo ukafanya vizuri sana, lakini wao wanaangalia vitu tofauti, kwa hiyo ni maamuzi tu. Mimi siwezi kuwa disappointed na tuzo, ni mamuzi ya kitaasisi tu,” alisisitiza.

Msanii kutoka Konde Gang, Harmonize amevunja kimya chake baada ya wimbo wake wa Single Again kutoteuliwa kuwania tuzo za BET katika kitengo chochote licha ya kuwa wimbo mkubwa wenye mafanikio kuntu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Waandaaji wa tuzo za BET za mwaka huu ambazo zitafanyika katika jimbo la Los Angeles nchini Marekani mwishoni mwa mwezi Juni walitoa orodha ya wasanii mbalimbali watakaowania tuzo za BET takribani wiki moja iliyopita, na kama ilivyotarajiwa, hakuna msanii hata mmoja kutoka ukanda wa Afrika Mashariki aliyejinafasi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maandalizi ya uzinduzi wa albamu yake ya tano na ya mwisho wikendi hii, Harmonize alisema kwamba tuzo ni maamuzi ya watu ambao mpaka wakuteue kuwani maanake tayari wamejiridhisha.

“Kiukweli mimi sijakatishwa tamaa, kwa sababu tuzo zozote ni maamuzi. Hata watu ambao wanateua wasanii kwenye tuzo wanakuwa wana vigezo vyao pia, unaweza ukawa unaona wimbo wako ni mzuri sana, kumbe wao wana vigezo tofauti wanaviangalia.”

“Unaweza ukatoa wimbo ukafanya vizuri sana, lakini wao wanaangalia vitu tofauti, kwa hiyo ni maamuzi tu. Mimi siwezi kuwa disappointed na tuzo, ni mamuzi ya kitaasisi tu,” alisisitiza.

Katika tuzo hizo za kitaifa, kitengo cha wasanii kutoka Afrika, walioteuliwa kuwania tuzo hizo ni mshindi wa Grammy kutoka Afrika Kusini, Tyla, wakali wa Nigeria, Burna Boy, Tems, Ayra Starr, Asake, Seyi Vibez, lakini pia wengine akiwemo Tyler ICU, Focalistic, Makhadzi.

Hayo yakijiri, katika rubaa za kimataifa, rapa wa Kanada, Drake anaongoza orodha ya wasanii watakaowania tuzo hizo, akiwa ameteuliwa katika vitengo 7 huku Nicki Minaj akiteuliwa kuwania katika vitengo 6.