Eric aikosoa kauli ya Otile kuwa hakuna msanii wa kimataifa Afrika Mashariki, amtaja Diamond

"Muziki sisi kama Wakenya tunao, ila kujiuza ndio tumelala… unajivaa vipi, unajibeba vipi… ukikutana na msanii wa Tanzania ni supastaa, Wakenya lazima waanze kuvaa vizuri,” Eric Omondi alisema.

Muhtasari

• Omondi aliwalaumu wasanii wa Kenya kwa kile alisema kuwa hawajui kujitangaza vilivyo ili kuonekana kuwa wasanii wanaomanisha kile wanachotaka katika tasnia ya muziki.

• Akiwalinganisha na wenzao wa Tanzania, Omondi alisema kuwa Wabongo wengi wanajua kuji’brand haswa katika mavazi ya fasheni za kuvutia kwenye video za miziki yao.

Eric Omondi amkosoa Otile kuhusu kauli yake kuwa hakuna wasanii wa kimataifa Afrika Mashariki.
Eric Omondi amkosoa Otile kuhusu kauli yake kuwa hakuna wasanii wa kimataifa Afrika Mashariki.
Image: Maktaba

Mwanaharakati Eric Omondi ameikosoa kauli ya Otile Brown kuwa hakuna msanii hata mmoja ukanda wa Afrika Mashariki ambaye amefanikiwa kuingia kaitka soko la kimataifa.

Itakumbukwa Otile Brown katika maojiano kwenye Obinna Show Live, alisema kwamba Afrika Mashariki bado tupo nyuma sana kimuziki, akisisitiza kwamba hakuna msanii hata mmoja amefaikiwa kuingia katika majukwaa ya kimataifa.

Omondi anahisi kwamba kauli ya Otile ilikosea kuwapa maua baadhi ya Wasanii wa Afrika Mashariki ambao kwa muda mrefu wameng’ang’ana na kuweka alama yao kimuziki katika soko la kimataifa kama vile Diamond Platnumz, msanii anayetajwa kuwa mtumbuizaji mkubwa kuwahi kutokea katika ukanda huo wa mataifa 8.

“Nafikiri ni Diamond peke yake ndiye amefanikiwa kuingia katika soko la kimataifa. Otile anaweza akawa aliteleza kwa kusema hakuna, ila sisi tunajua kuna mmoja – Diamond Platnumz,” Eric Omondi alisema.

Alimsifia Diamond kwa juhudi zake si tu kwenda katika soko la muziki la kimataifa bali pia amefanikiwa kuwavuta baadhi ya wasanii wa kimataifa kuja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Diamond ameenda kimataifa laini pia amewaleta wasanii wa kimataifa Afrika Mashariki. Yeye peke yake, hakuna mwingine,” alisisitiza.

Omondi aliwalaumu wasanii wa Kenya kwa kile alisema kuwa hawajui kujitangaza vilivyo ili kuonekana kuwa wasanii wanaomanisha kile wanachotaka katika tasnia ya muziki.

Akiwalinganisha na wenzao wa Tanzania, Omondi alisema kuwa Wabongo wengi wanajua kuji’brand haswa katika mavazi ya fasheni za kuvutia kwenye video za miziki yao.

“Ukiziona video za Tanzania ni za kimataifa, Diamond anafanya video kwa fasheni za kuvutia. Hiyo ndio showbiz sasa. Tanzania hawatushindii muziki, wanatushindia showbiz na uwekezaji katika muziki. Muziki sisi kama Wakenya tunao, ila kujiuza ndio tumelala… unajivaa vipi, unajibeba vipi… ukikutana na msanii wa Tanzania ni supastaa, Wakenya lazima waanze kuvaa vizuri,” Eric Omondi alisema.

Kama mmoja ambaye amejumuika na Harmonize na Diamond, Eric Omondi aliweza kuwalinganisha na kusema;

“Wale ni kama baba na mwanawe, tofauti ni kwamba Diamond ni mfanyibiashara ambaye amekomaa sana, ameelewa shoo na biashara, ako na uzoefu kadhaa. Harmonize kwa upande wake ameelewa muziki, sana sana wa Bongo, anaelewa muda upi wa kutoa ngoma ya maudhui gani,” aliwalinganisha.

Kuhusu uhusiano wake na Tanzania, Eric Omondi alisema kuwa anamheshimu sana Diamond kwa kuwa ndiye mtu wa kwanza kumualika na kumtambulisha Tanzania wakati wa tamasha la Zari White Party, kipindi hicho wakiwa wapenzi.