Wanawe Esther Musila wafichua sifa zake za kipekee na za baba yao wa kambo Guardian Angel

Glenn na Gilda walimtambua mama yao Esther Musila kuwa ndiye mwenye mahaba zaidi.

Muhtasari

•Glenn na Gilda walibainisha kuwa kati ya wazazi wao, Guardian Angel ndiye aliyekuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kumwambia mwenzake "Nakupenda."

•Glenn na Gilda pia walifichua kwamba Guardian Angel ndiye anayejifanya sana "kama mtoto" wakati akiwa mgonjwa

Guardian Angel, mkewe Esther Musila na watoto wao Glenn na Gilda Naibei
Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Guardian Angel, mkewe Esther Musila na watoto wao wakubwa Glenn Naibei na Gilda Naibei walishiriki katika mchezo uliohusisha kutambua sifa za kipekee ambazo kila mzazi anamiliki.

Katika mchezo huo uliopewa jina la ‘Wafahamu wazazi wako na G’s’, Glenn na Gilda walihitajika kutambua ni nani kati ya mama yao na baba yao wa kambo ana sifa fulani iliyosomwa kwao kwenye simu.

Swali la kwanza lilikuwa ni kuhusu ni mzazi yupi mcheshi zaidi na wote wabili walinyoosha vidole vyao kwa Guardian Angel. Katika swali la pili, walimtambua mama yao Esther Musila kuwa ndiye mwenye mahaba zaidi.

Glenn na Gilda walibainisha kuwa baba yao wa kambo Guardian Angel ndiye mvumilivu zaidi kuliko mama yao. Hata hivyo walidokeza kuwa Bi Musila ndiye mpishi bora kati ya wazazi hao wao wawili.

Wawili hao ambao wana umri wa ujana walibainisha kuwa kati ya wazazi wao wawili, Guardian Angel ndiye aliyekuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kumwambia mwenzake kuwa "Nakupenda."

Walibainisha zaidi kwamba mama yao ndiye huchukua muda mrefu zaidi kujiandaa asubuhi. Bi Musila pia alitambuliwa kuwa ndiye mkaidi zaidi kati ya wanandoa hao.

Glenn na Gilda pia walifichua kwamba Guardian Angel ndiye anayejifanya sana "kama mtoto" wakati akiwa mgonjwa. Hata hivyo, walibainisha kuwa hakuna kati ya wazazi wao wawili ambaye ni mchafu.

Esther Musila pia alichaguliwa na watoto wake kuwa ndiye anayefanya mazoezi zaidi na pia anayehitaji umakini zaidi.

Mwimbaji Guardian Angel na Esther Musila wamekuwa kwenye ndoa rasmi kwa takriban mwaka mmoja. Wawili hao walifunga ndoa mapema mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa takriban miaka miwili.