Diamond ashindwa kuficha furaha baada ya Jesse Lingard kufurahia muziki wake

‘Shu’ ni wimbo wa hivi punde zaidi wa Diamond na ni ushirikiano wa amapiano na mwimbaji wa Afrika Kusini, Chley Nkosi

Muhtasari

•Lingard alishiriki wimbo wa Diamond ‘Shu’ kwenye stori zake za Snapchat na kuuambatanisha na emoji za mtu anayecheza densi, kiashiria kuwa anaupenda na kufurahia wimbo huo.

•Wimbo huo uliachiwa takriban mwezi mmoja uliopita na tayari umepata watazamaji zaidi ya milioni 5.2 kwenye mtandao wa YouTube.

amefurahia baada ya Jesse Lingard kushare wimbo wake.
Diamond Platnumz amefurahia baada ya Jesse Lingard kushare wimbo wake.
Image: INSTAGRAM//

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz alikuwa mwenye bashasha tele baada ya mwanasoka mashuhuri wa Uingereza, Jesse Lingard kumuonyesha upendo kwa kushare moja ya nyimbo zake za hivi majuzi kwenye Snapchat.

Lingard ambaye kwa sasa anafanya mazoezi na klabu yake ya zamani ya West Ham yenye maskani yake jijini London alishiriki wimbo wa Diamond na Chley ‘Shu’ kwenye stori zake za Snapchat na kuuambatanisha na emoji za mtu anayecheza densi, kiashiria kwamba anaupenda na kufurahia wimbo huo.

Bosi huyo wa WCB pia alichapisha rekodi ya skrini ya stori ya Lingard ya Snapchat kwenye Instastories zake na kumtaja mchezaji huyo wa Kiingereza ili kuonyesha shukrani.

"@jesselingard👑🔥," Diamond aliandika.

‘Shu’ ni wimbo wa hivi punde zaidi wa mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz na ni ushirikiano wa amapiano na mwimbaji wa Afrika Kusini Chley Nkosi. Wimbo huo uliachiwa takriban mwezi mmoja uliopita na tayari umepata watazamaji zaidi ya milioni 5.2 kwenye mtandao wa YouTube.

Siku chache zilizopita, klabu ya soka ya Ufaransa, PSG walipakia video ikionesha hali ya anga katika uwanja wao Parc des Princes na katika video hiyo, wakaamua kutumia wimbo huo huo wa Diamond na Chley 'Shu'.

Kitendo cha PSG kilionekana kuzua kugombana baina ya mashabiki wa muziki wa Amapiano barani Afrika baada ya vigogo hao wa soka wa Ufaransa kudaiwa kuwakwepa wasanii wote wa Amapiano kutoka Afrika kusini – nchi ya asili ya Amapiano – na badala yake kumchagua Diamond Platnumz kutoka Tanzania.