Nabii Bahati! Mwimbaji Size 8 asimulia jinsi Bahati alivyomuokoa kutokana na kukosa watoto

Size 8 alifichua kuwa Mungu alizungumza naye kupitia Bahati kuhusu jinsi shetani almpangia mfululizo wa kuharibika kwa mimba.

Muhtasari

•Size 8 alifichua kwamba Bahati ana kipawa cha unabii ambacho kilimsaidia kuepuka maisha ya kilio na mahangaiko miaka iliyopita.

•“BAHATI Mungu alikutumia kweli! Ninaamini atakutumia zaidi! Siku zote nitakuita NABII BAHATI MTUMISHI WA MUNGU ALIYE JUU,” alisema.

DJ Mo, Size 8, Diana Marua, Bahati
Image: HISANI

Huenda mhubiri na mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili Linet Munyali almaarufu Size 8 hangekuwa na mtoto hata mmoja leo kama si unabii wa Bahati takriban mwongi mmoja uliopita.

Wakati akijibu chapisho la Bahati kwenye Instagram siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto wawili alifichua kwamba mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili ana kipawa cha unabii ambacho kilimsaidia kuepuka maisha ya kilio na mahangaiko miaka iliyopita.

Katika jibu lake, Size 8 alifichua kuwa Mungu alizungumza naye kupitia Bahati akamueleza jinsi shetani alivyompangia mfululizo wa kuharibika kwa mimba ili asipate watoto.

“Halo mtu wa Mungu nabii @bahatikenya... Hapa ndipo nyumbani kwako kaka. Nakiheshimu na kukitambua kipawa na uzao wa Mungu ulio ndani yako nabii wa Mungu aliye juu.. Nakumbuka mwaka 2013 Mungu alizungumza nawe kuhusu ajenda ya shetani ili kuhakikisha kwamba sipati watoto kwa njia ya kuharibika kwa mimba, ukaniambia. “size 8 REBORN omba omba sana” na nilichukua neno lako nabii na nina watoto 2,” Size 8 alisimulia.

Mke huyo wa DJ Mo alibainisha kuwa Bahati bado ana mengi ya kutoa katika tasnia ya injili na kuweka wazi kuwa daima atamtambua kama nabii kila wakati.

“BAHATI Mungu alikutumia kweli! Ninaamini atakutumia zaidi! Siku zote nitakuita NABII BAHATI MTUMISHI WA MUNGU ALIYE JUU,” alisema.

Size 8 alikuwa akitoa maoni yake kuhusu chapisho la mwimbaji huyo ambapo alikuwa akiuza wimbo wake mpya wa Injili ‘Unarudi Lini.’

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili na mume wake DJ Mo wamejaliwa watoto wawili kufikia sasa. Takriban miaka miwili iliyopita, wawili hao kwa bahati mbaya walipoteza ambaye angekuwa mtoto wao wa tatu baada ya Size 8 kupoteza mimba.

Mhubiri huyo tayari alikuwa amebeba ujauzito wake kwa miezi mitano wakati ambapo aliupoteza mnamo Oktoba 2,  2021.

Akizungumza tukio hilo mapema mwaka huu , alifichua kwamba wakati huo alikuwa amepoteza matumaini kabisa ya kuwahi kuwa mjamzito tena. Alisema alikuwa karibu kupoteza maisha pia kwani shinikizo la damu lilikuwa limemshambulia vibaya.

"Nikikumbuka siku hii, tarehe 2 Oktoba 2021. Nilikuwa nimetoka tu kupoteza ujauzito wa miezi 5, pia nilipoteza matumaini kabisa ya kupata ujauzito wowote katika siku za usoni na nilikuwa nikipigania maisha yangu, karibu nipoteze maisha yangu kutokana na shinikizo la damu kupindukia," alisema na kuambatanisha ujumbe huo na picha ya kumbukumbu iliyomuonyesha akiwa amelazwa hospitalini.

Mhubiri huyo alisema ni kwa neema ya Mungu kuwa alinusurika kusimulia na hiyo akamshukuru kwa kuokoa maisha yake.

Aliweka wazi kuwa tukio hilo ni moja tu ya sababu nyingi zinazomfanya sasa amtumikie Bwana kama mchungaji.

"Woi Baba yangu wa Mbinguni nakushukuru kwa kuhifadhi maisha yangu. Nisaidie kutumia zawadi hii ya uhai ulionipa kwa utukufu wako," alisema.