"Mimi bado ni mtoto!" Nyota Ndogo ajibu kwa hasira baada ya kukejeliwa ni mzee sana kuweza kuzaa

Alieleza kuwa mwanamke ambaye bado ana hedhi kila mwezi anaweza kujifungua bila kujali umri wake.

Muhtasari

•Wakenya walichukua fursa kutoa maoni, wengi wao wakimpongeza huku wengine wakimkosoa bila aibu kuhusu muda wa ujauzitowake.

•Nyota Ndogo aliwakashifu vikali wale wanaozungumza vibaya kuhusu ujauzito wake badala ya kumpongeza kwa kuwa mjamzito.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki mzaliwa wa Pwani Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amewajibu kwa hasira wakosoaji wa ujauzito wake wa sasa.

Nyota Ndogo alifichua ujauzito wake mapema wiki hii na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wakachukua fursa kutoa maoni, wengi wao wakimpongeza huku wengine wakimkosoa bila aibu kuhusu muda wa ujauzitowake.

Huku akiwajibu wenye chuki kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 alidokeza kuwa bado ni mchanga sana na ana uwezo wa kuzaa.

“Wenye kusema mimi ni mzee sifai kuzaa, siku ya kujifungua  njooni musukume nyinyi maana nyie ndio mna nguvu za kusukuma. Kwanza mimi am only 42 bado mchanga sana. Happy birthday to me, oh sorry pongezi kwangu,” Nyota Ndogo alisema.

Katika video ambayo pia alishiriki, alieleza kuwa mwanamke ambaye bado ana hedhi kila mwezi bado anaweza kujifungua bila kujali umri wake.

Wakati huo huo, aliendelea kuwakashifu vikali wale wanaozungumza vibaya kuhusu ujauzito wake badala ya kumpongeza kwa kuwa mjamzito miaka tisa baada ya kufunga ndoa na mume wake wa Kidenmark, Henning Neilsen.

“Asanteni sana kwa wanaosema hongera maana najua imetoka kwa roho zenu. Ila wale wenye kusema wewe utazaa vipi, wewe wataka kuja kunikamua? Kama Mwenyezi Mungu kanipa ujauzito, anajua vile nitajifungua. Kama unaona inakuwasha, njoo unisaidie kusukuma siku nitakapokuwa naumwa na uchungu. Jamani mimi bado mtoto. Mwanamke wa miaka 70 anashika ujauzito, mimi ni nani. Mimi bado ni mtoto,” alisema.

Hapo awali, mwanamuziki huyo mkongwe aliwashukuru wale wote waliompongeza kufuatia taarifa za hivi punde za ujauzito wake.

Katika taarifa yake siku ya  Alhamisi jioni, mama huyo wa watoto wawili hata hivyo aliweka wazi kuwa amepigwa marufuku kuzungumza kuhusu ujauzito wake na vyombo vya habari au mamlaka na mume wake Henning Neilsen.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 alisema ameruhusiwa tu kujizungumzia yeye na muziki wake na sio ujauzito hadi atakapojifungua.

“Asanteni kwa hongera zenu, lakini media mtanisamehe mume wangu amesema hataki kuona kwenye kituo chochote cha radio TV ama polisi nikiongelea hali yangu. Kwa hiyo endapo nitatoa interview iwe ya mimi na mziki wangu na sio ujauzito wangu, ama nisitoe mpaka nijifungue,” Nyota Ndogo alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Nyota Ndogo ambaye sasa anaendesha hoteli mjini Voi aliambatanisha taarifa yake na video inayomuonyesha akinengua mauno huku wimbo wa kumshukuru Mungu ukicheza. Katika video hiyo, tumbo lake lilionekana kuchomoza sana, thibitisho kwamba kwa kweli amebeba ujauzito wa mtoto wake wa tatu.

Nyota Ndogo alitangaza habari za ujauzito wake Jumanne kutumia picha ambayo  ilimuonyesha akiwa ameshikilia tumbo lake lililochomoza.Hata hivyo, hakufichua maelezo yoyote zaidi katika sehemu ya maelezo na aliwaacha mashabiki kukisia tu.