Mwanadada wa Bomet anayedaiwa kusimamisha harusi siku kabla hatimaye aeleza kilichotokea

Bi Nelly Chepkoech hatimaye ameibuka na kuweka mambo bayana kuhusu sababu ya harusi yao kutofanyika.

Muhtasari

•Ndoa ya Nelly na Amos ilisitishwa siku moja kabla ya kufanyika, na kusababisha minong'ono na mkanganyiko miongoni mwa wahusika.

•Nelly alikanusha madai ya kutoroka nyumbani ili kukwepa harusi yake, akibainisha kuwa bado yuko nyumbani kwa mzazi wake.

Bi Nelly Chepkoech
Image: HISANI

Bi Nelly Chepkoech, mwanadada kutoka Kaunti ya Bomet ambaye anadaiwa kusimamisha harusi yake siku moja tu kabla ya tarehe iliyowekwa kufanyika hatimaye ameibuka ili kutupilia mbali madai hayo.

Nelly na mumewe Amos walipaswa kufunga ndoa rasmi mnamo Jumamosi, Desemba 11 katika Kanisa la AGC Kapsoyo lakini mipango ya harusi ilisitishwa siku moja kabla ya sherehe hiyo kufanyika, na kusababisha minong'ono na mkanganyiko miongoni mwa wahusika.

Gumzo za kundi la WhatsApp miongoni mwa wanachama wa kamati ya kupanga harusi zilivuja kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha uvumi na shutuma zaidi miongoni mwa wanamitandao, wengi wao wakiwa wanamnyooshea vidole Nelly.

Wakati akizungumza na vyombo vya habari siku ya Jumamosi, mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 23 hata hivyo alikanusha kughairi harusi yake na kudai kuwa ulikuwa uamuzi wa kanisa kuahirisha harusi hiyo kutokana na kuchelewa kwa stakabadhi kadhaa.

“Leo (Jumamosi) ingekuwa siku yangu ya harusi lakini tulifika tukaambiwa harusi haiwezi jana kwa sababu ya kuchelewa kwa baadhi ya barua. Lakini tulikuwa tukisubiri siku kwa hamu,” Nelly alisema.

Mrembo huyo pia alikanusha madai ya kutoroka nyumbani ili kukwepa harusi yake, akibainisha kuwa bado yuko nyumbani kwa mzazi wake.

Alifichua kuwa kulitokea mkanganyiko na hisia zilipanda baada ya kufahamishwa kuwa tukio lao kubwa halingefanyika jinsi walivyopanga. Hata hivyo aliweka wazi kuwa yuko tayari kufunga ndoa na Amos kwani walihakikishiwa kutengewa siku nyingine ya harusi.

“Kila mtu alikuwa na machozi, kila mtu alikuwa analia. Mimi niko nyumbani sijapotea. Bado niko nangoja siku ambayo tuliambiwa tutaitwa. Niko tayari kwa siku hiyo,” alisema.

Aliongeza, “Tunangoja reverend atuambie siku tuendelee na harusi. Sijasema aliifutilia mbali. Iliahirishwa."

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakijadiliana vikali kuhusu kuahirishwa kwa harusi ya Nelly na Amos tangu gumzo la kundi la WhatsApp kufichuliwa. Kumekuwa na kila aina ya uvumi na shutuma huku nyingi zikionekana dhidi ya mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 23.

Harusi iliyoahirishwa ilipaswa kurasimisha uhusiano wa wanandoa hao wa takriban miezi tisa.