"Ningekuwa Mkenya!" Rayvanny afichua sababu yeye na Diamond walijaribu kubadili uraia kuwa Wakenya

Alifichua kuwa Diamond alipendekeza wabadili uraia wao baada ya serikali ya Tanzania kuwafungia kufanya muziki.

Muhtasari

•Rayvanny amefunguka kuhusu jaribio lake na Diamond Platnumz lisilofanikiwa la kubadilisha uraia na kuwa Wakenya.

•Mabadiliko ya uraia hata hivyo hayakuhitimishwa kwani tatizo ambalo waimbaji hao walikuwa nalo na serikali lilitatuliwa baadaye.

Diamond na Rayvanny
Diamond na Rayvanny
Image: Instagram

Mwanamuziki maarufu wa Tanzania Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny amefunguka kuhusu jaribio lake lisilofanikiwa la kubadilisha uraia na kuwa Mkenya.

Wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, Rayvanny alifichua kuwa bosi wake wa zamani wa WCB, Diamond Platnumz alipendekeza wabadili uraia wao baada ya serikali ya Tanzania kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuwafungia kufanya muziki au kutumbuiza kwa sababu ya wimbo uliopigwa marufuku 'Mwanza.'

Kisa hicho kilitokea mwaka wa 2018 baada ya waimbaji hao wawili kutumbuiza wimbo huo uliopigwa marufuku kwenye Wasafi Festival 2018.

“Nilikuwa na stress. Tulikuwa tumefungiwa kufanya muziki. Tuliperform ule wimbo wa Mwanza ambao ulifungiwa. Baada ya kufungiwa, tukawa tumefungiwa kufanya muziki na nini, sasa hapo Diamond akanipa idea, ‘unaonaje tuwe Wakenya. Tubadilishe uraia,” Rayvanny alisema.

Bosi huyo wa lebo ya Next Level Music alifichua kuwa kufuatia wazo la Diamond, walijaribu kuanza mchakato wa kubadilisha uraia wakati wa ziara yao iliyofuata nchini Kenya.

Mabadiliko ya uraia hata hivyo hayakuhitimishwa kwani tatizo ambalo waimbaji hao wawili walikuwa nalo na serikali lilitatuliwa baadaye.

“Baadaye tulimaliza. Serikali ilituachia huru na tukawa tunaendelea na kazi zetu. Kwa hiyo zoezi letu lilisimama. Tulikuwa tumekuja kutafuta urais tuwe Wakenya. Kama tungeendelea kuzuiwa ningekuwa Mkenya lakini tulisuluhisha,” alisema.

Mkali huyo wa bongo fleva alibainisha kuwa wazo la kubadili uraia liliwajia kwa sababu ya mkanganyiko uliojitokeza baada ya wao kufungiwa.

Mwishoni mwa mwaka wa 2018, Diamond Platnumz na Rayvanny walifungiwa kufanya shoo yoyote ndani na nje ya Tanzania na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Baraza hilo lilisema marufuku hiyo ya muda usiojulikana ingeanza kutekelezwa mara moja baada ya wawili hao kucheza wimbo 'Mwanza' wakati wa ziara yao mjini Mwanza.

Hapo awali, wasanii hao walikuwa awali wametakiwa kuuondoa wimbo wao kwa jina 'Mwanza' kutoka kwenye mitandao ya kijamii, lakini wimbo huo ulindelea kuwepo kwenye YouTube.Pia waliendelea kuucheza kwenye matamasha.

Basata walitangaza kuufungia wimbo wa Mwanza mnamo Novemba 2018 kwa kile walichosema ni "kwa kubeba maudhui machafu."