"Alichukua simu akilia!" Pritty Vishy ahuzunika baada ya mamake kupata ajali

Kulingana na Pritty Vishy, ​​gari la mamake lilitua kwenye mtaro baada ya breki kukosa kufanya kazi.

Muhtasari

•Mamake Pritty Vishy alikuwa akiendesha gari dogo jeupe kuelekea nyumbani kwa bintiye wakati alihusika katika ajali.

•"Alikuwa analia akisema amepata ajali. Nilienda katika eneo la tukio haraka. Kwa bahati nzuri hakuwa amejeruhiwa sana,” alisema.

Pritty Vishy na mama yake.
Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Mtayarishaji maudhui Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy alibaki mwanamke mwenye wasiwasi baada ya mama yake ambaye alirejea Kenya hivi majuzi kutoka Saudi Arabia kuhusika katika ajali ya barabarani.

Mamake Pritty Vishy alikuwa akiendesha gari dogo jeupe kuelekea nyumbani kwa mpenzi huyo wa zamani wa Stevo Simple Boy wakati alihusika katika ajali mahali pasipojulikana.

Kulingana na Pritty Vishy, ​​gari la mamake lilitua kwenye mtaro baada ya breki kukosa kufanya kazi.

“Kilichotokea, breki zake zilianza kusumbua na hivyo ndivyo alipoteza mwelekeo akajipata kwa shimo,” Pritty Vishy alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Aliongeza, "Lakini angalau anapata nafuu kiakili kwa sababu amekuwa hayuko sawa."

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22 aliambatanisha taarifa yake na video ya gari la mamake lililopata ajali likiwekwa kwenye lori kwa ajili ya kusafirishwa.

Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Huku akishiriki maelezo zaidi ya ajali hiyo, mpenzi huyo wa zamani wa mwimbaji Stevo Simple Boy alitoa simulizi ya jinsi mambo yalivyojiri kabla ya tukio hilo la kutisha.

“Kwa hiyo nilimpigia simu mama yangu na kumwambia aje kwangu (Alhamisi) kwa sababu nilitaka anipeleke mahali siku iliyofuata (Ijumaa) akakubali kuja lakini alikuja mapema. Lakinis siku nzima akakuwa busy na tukabadilisha mpango wa yeye kuja hio Thursday  kwani amekuwa busy tu akuje Friday asubuhi. So mwendo wa saa nne usiku akanipigia akaamua ameamua kutoka kwa hiyo siku kwa sababu hataki kunichelewesha siku ifuatayo na nikasema ni sawa,” Pritty Vishy alisimulia.

Aliendelea, “Nilimsubiri kama masaa mawili ikabidi nipige simu nijue amefika wapi maana nilishangaa juu yeye hufika ndani ya dakika 30. Hakuchukua simu yake lakini niliendelea kupiga, bila kujua wakati hakuwa anashika alikuwa anang’ang’ana kutoka kwa gari.”

Vishy alifichua kuwa hatimaye mamake aliweza kupokea simu hiyo baada ya kutoka nje ya gari na kumfahamisha kuwa alikuwa amepata ajali

“Mwishowe alichukua na alikuwa analia akisema amehusika katika ajali. Nilienda katika eneo la tukio haraka. Kwa bahati nzuri hakuwa amejeruhiwa sana,” alisema.

Mamake Pritty Vishy alirejea Kenya mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kufanya kazi nchini Saudi Arabia kwa takriban miaka mitano.