Mr Seed alazimika kuomba msamaha baada ya matamshi yake kumkasirisha sana mkewe

Mwanamuziki huyo ameeleza majuto yake makubwa na kumuahidi mke wake mrembo kuwa atabadilika.

Muhtasari

•Mr Seed amenyenyekea na kuomba msamaha kutoka kwa mkewe Nimo Gachuiri baada ya wawili hao kutofautiana kuhusu matamshi tata ya hivi majuzi.

•Seed ameeleza zaidi kujitolea kwake katika uhusiano wao na kukiri kuhusu upendo wake mkubwa kwa mama huyo wa mtoto wake.

Mwimbaji Mr Seed amemuomba msamaha mke wake
Mwimbaji Mr Seed amemuomba msamaha mke wake
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili na mapenzi Moses Tarus Omondi almaarufu Mr Seed amenyenyekea na kuomba msamaha kutoka kwa mkewe Nimo Gachuiri baada ya wawili hao kutofautiana kuhusu matamshi tata ya hivi majuzi.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mr Seed aliomba radhi kwa matamshi yake kuhusu ndoa na mahusiano ambayo alitoa kwenye podikasti moja ya humu nchini na kubainisha kwamba hakukusudia kumuumiza mkewe.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Dawa ya Baridi’ pia alitumia fursa hiyo kueleza majuto yake makubwa na kumuahidi mke wake mrembo kuwa atabadilika.

"Mpendwa Nimo, ninaomba msamaha wa dhati kwa maudhi yoyote yasiyokusudiwa ambayo matamshi yangu ya hivi majuzi kuhusu ndoa na mahusiano yanaweza kuwa yamesababisha," Mr Seed alisema siku ya Jumatano adhuhuri.

Aliongeza, “Natambua sasa kwamba maneno yangu hayakuendana na heshima niliyo nayo kwako. Hisia zako ni muhimu sana kwangu, na nimejitolea kuwa mwenye kufikiria zaidi katika mazungumzo yangu kusonga mbele."

Aidha, Seed ameeleza zaidi kujitolea kwake katika uhusiano wao na kukiri kuhusu upendo wake mkubwa kwa mama huyo wa mtoto wake.

"Ninathamini uhusiano wetu sana na ninajutia usumbufu wowote ambao maneno yangu yanaweza kuletwa kwako au kwa mtu mwingine yeyote. Kwa upendo,"

Msanii huyo mahiri alitokea kwenye podcast moja ya humu nchini na kuzungumzia masuala ya mahusiano ambapo alisema kwa tajriba yake kwenye ndoa, mwanamume ni kiumbe ambaye anaweza akawa kwenye mahusiano na mwanamke kwa miaka 3 lakini bado akawa anawazia kuoa mwanamke mwingine.

Mr Seed alisema kwamba wanaume kwa kawaida ni wa mitala na kwamba mwanamke kuishi na yeye kwa muda mrefu si kigezo cha kumfanya kuhisi kwamba ameshinda, kwani anaweza amka siku moja tu agundue mume wake anapanga kufunga harusi na mwanamke mwingine hali ya kuwa yeye bado yupo.

“Hebu niambie, sisi wanaume tuna akili. Ninaweza kuwa na wewe kwenye uhusiano kwa miaka kama 3 unaelewa? Miaka mitatu tu ya mimi kukutazama nikijua vizuri huna ninachokitaka.”

“Kwa hivyo niko hapo halafu siku moja unaamka na kukuta jamaa tayari ameshaandaa harusi kwa sababu msichana huyu tayari alidhani alikuwa mshindi. Tuna marafiki wengine wa kike sawa? Miongoni mwa marafiki hao, tunaangalia kati yao kuona nani ni mke mzuri. Labda hata ni rafiki yako mkubwa,” Mr Seed alisema.

Aliongeza "Wanaume wameumbwa kuwa na wake wengi."

Matamshi haya yalionekana kumuudhi mno mkewe Nimo ambaye kupitia Instastori zake alimkanda vikali akisema kwamba matamshi kama hayo hayafai kutoka kwa kinywa cha mwanaume anayejua kwamba yuko katika ndoa imara.

"Kwa hivyo niliona kipande kidogo cha podikasti iliyofanywa na Mr Seed, akisema chochote alichokuwa akisema. Hata sikumaliza kuitazama. Nilikasirika. Basi nikamgeukia na kumuuliza, hizi sasa ni nini unasema hakika. Kitu kingine nilichosema lazima watu wafikiri mimi ni mjinga! Kwa hivyo alikuwa kama unapaswa kutazama podikasti nzima na walichagua sehemu hiyo pekee ili iweze ku-trend,” Nimo aliandika.

"Ninachotaka kusema ni kama ni kwa ajili ya mapenzi, lilikuwa jambo lisilo na hisia kusema wakati uko katika uhusiano wa kujitolea," alisema zaidi.

Kwa tathmini ya haraka, Nimo alikuwa tayari ameshakatisha urafiki kwa mumewe katika mtandao wa Instagram.