•Nyota Ndogo alibainisha kuwa mzungu huyo ndiye mshirika wake wa maisha aliyeteuliwa na akamshukuru kwa kumkubali pamoja na watoto wake.
•Aliendelea kumhakikishia mzungu huyo kuhusu mapenzi yake makubwa kwake na kuahidi kutomuacha kamwe.
Mwimbaji mkongwe wa Kenya Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo mnamo siku ya Ijumaa alimsherehekea mumewe kwa ujumbe mzuri na wa kusisimua alipokuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.
Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, mama huyo wa watoto wawili alichapisha picha yake na mumewe Henning Nielsen na kutumia chapisho hilo kumsherehekea mzungu huyo kwa kuwa katika maisha yake.
Katika ujumbe wake, alibainisha kuwa raia huyo wa Denmark ndiye mshirika wake wa maisha aliyeteuliwa na akamshukuru kwa kumkubali pamoja na watoto wake.
“Ubavu wangu wa pili ni wewe, wewe ndio MUNGU aliniandikia. Uliamua utanipokea na wanangu ukanipokea nilivyo, yani unasemaga ukiwa na mimi huboeki,” Nyota Ndogo aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Aliendelea kumhakikishia mzungu huyo kuhusu mapenzi yake makubwa kwake na kuahidi kutomuacha kamwe.
Aidha, mwimbaji huyo mzaliwa wa Pwani aliapa kwa kejeli kumroga mume ikiwa atafikiria kugura ndoa yao.
“Mume wangu nakupenda sana, labda uniwache wewe lakini mimi siwezi kukubali kukupoteza. Ukileta ujinga nakuroga unarudi kwa laini,” aliandika,
Aliongeza ,”Kheri ya siku ya kuzaliwa mume wangu Henning. Wapendwa,. hii kitu imenishinda kujieleza kidhungu, munaweza ku translate akija asome vizuri aelewe. Haya wasomi njooni.”
Nyota Ndogo na Bw Henning Nielsen wamekuwa kwenye ndoa ya mbali kwa takriban miaka sita. Wanandoa hao wawili walifunga pingu za maisha mwezi Mei 2016 baada ya kuchumbiana kwa muda.
Mapema mwaka jana Nyota Ndogo alifichua kuwa ilichukua mwaka mmoja kwa yeye kujibu ombi la ndoa la mumewe huyo mzungu.