Wimbo wenye utata wa Embarambamba kuhusu kifo cha Kelvin Kiptum wazua hisia mseto (+video)

Mwimbaji huyo alimuomboleza mshikilizi huyo wa Rekodi ya Dunia katika mbio za marathon kwa maneno ya kutatanisha.

Muhtasari

•Embarambamba anaonekana akiwa amekaa kwenye maji chafu huku sehemu kubwa ya mwili wake pia ikiwa imetapakwa matope.

•Mwimbaji huyo alionekana kuigiza kila kitu ambacho alikuwa anazungumza kuhusu alipokuwa akiimba.

Image: HISANI

Video ya mwimbaji wa Kisii Christopher Mosioma almaarufu Embarambamba akimwomboleza marehemu mwanariadha Kelvin Kiptum katika wimbo wenye utata imekuwa ikivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia tofauti kutoka kwa wanamitandao.

Katika video hiyo yenye urefu wa zaidi ya dakika tatu, mwanamuziki huyo aliyezingirwa na utata mwingi anaonekana akiwa amekaa kwenye maji chafu huku sehemu kubwa ya mwili wake pia ikiwa imetapakwa matope

Mwimbaji huyo anasikika akiimba wimbo akidai kumuomboleza mshikilizi huyo wa Rekodi ya Dunia katika mbio za marathon kwa maneno ya kutatanisha ambayo yamewaacha watumiaji wengi wa mtandao wakiuliza ikiwa ni yuko sawa. 

Katika mwanzo wa wimbo, anasikika akieleza jinsi marehemu Kiptum alifariki kutokana na ajali na akizungumzia jinsi alivyohuzunishwa na kifo chake.

“Sijafurahishwa na Kelvin, nalia (*5) .. Kelvini Kelvini, Kelvini amekufa. Gari liligonga mti, Kelvini amekufa. Sina furaha, hapa kutoka Kenya. Wakenya tuseme nini? Wakenya tukae wapi?,” Embaramba aliimba.

Aliendelea kuimba kuhusu jinsi mwanariadha huyo alivyojituma kabisa hadi kuvunja rekodi kwenye majukwaa ya kimataifa.

“Wakenya tuhameni, Wakenya tuseme nini? Wakenya tukae wapi?” aliimba.

Mwimbaji huyo alidai kuwa Kiptum alikuja Kenya kusalimia familia yake alipohusika kwenye ajali mbaya iliyosababisha kifo chake.

“Kelvin amekufa! Alikuwa mkimbiaji, wewe Kelvini. Kelvini Kelvini, umewacha ukoo wapi? Kelvini Kelvini, umeacha bibi wapi? Kitanda ulikuwa unalala, umekiacha wapi?

Kelvini ugali ulikuwa unakula , umewacha wapi? Gari kwenda poo,ikagonga Kelvini pu! Gari ikapata ajali, gari kwenda raaa, ikagonga mti Kelvini akakufa,” Embarambamba aliimba.

Mwimbaji huyo alionekana kuigiza kila kitu ambacho alikuwa anazungumza kuhusu alipokuwa akiimba.

Video hiyo imepokelewa na Wakenya kwa hisia tofauti, wengine wakionekana kumkosoa mwimbaji huyo, wengine wakitaja kitendo chake kuwa cha kipumbavu huku wengine wakijiuliza iwapo yuko sawa kiakili.

Tazama maoni ya baadhi ya watumiaji wa mtandao wa kijamii wa X:-

Talai: Huyu Embarambamba ako na ujinga gani Hii sasa 😡 people are mourning Kelvin Kiptum & he is busy making fun.

Kawangware finest: When must stop this embarambamba? Anyways, let the mourning, mourn their way.

TheRealMvitaOne: Embarabamba kwa ubora wake mourning our departed champ . Kuna kitu anavuta na kina steam mbaya sana🤣🤣🤣

Lord if Ricks: Is Embarambamba mentally upright?

Kimani Karuga: Embarambamba should be stripped of Kenyan citizenship.