Director Trevor amtambulisha mrithi wa Mungai Eve, wakati halisi walioachana wafichuliwa

Mwanadada mwingine atakuwa sura ya Kenya Online Media ambayo awali ilijulikana kama Mungai Eve Media.

Muhtasari

•Bi Rael Wangari atachukua nafasi ya Eve Mungai katika iliyokuwa Mungai Eve Media ambayo sasa imebadilishwa kuwa Kenya Online Media.

•Ilifichuliwa kwamba Director Trevor na Mungai Eve hawajakuwa pamoja kwa takriban mwaka mmoja kwani walitengana Februari mwaka jana.

Mungai Eve, Director Trevor, Rael Wangari
Image: INSTAGRAM

Ni rasmi kuwa Bi Rael Wangari atachukua nafasi ya mwanahabari Eve Mungai katika iliyokuwa Mungai Eve Media ambayo sasa imebadilishwa kuwa Kenya Online Media.

Mrembo huyo alitambulishwa kuwa sura mpya ya Kenya Online Media kupitia video ya YouTube siku ya Jumanne ambapo alidokeza kuhusu jukumu lake jipya.

Huku akijitambulisha kwenye video hiyo, Bi Wangari aliwaomba mashabiki wa iliyokuwa Mungai Eve Media kuendelea kuwapa sapoti. Naye aliahidi kuwapa maudhui zaidi kwa ushirikiano wa washiriki wengine wa timu ya Kenya Online Media akiwemo Director Trevor mwenyewe na Captain Nyota.

"Kenya Online Media imejitolea kukupa yaliyomo kila saa. Chai, udaku, mahojiano ya watu mashuhuri na masasisho ya watu mashuhuri yatahutolewa kwako mara kwa mara,” Bi Rael Wangari alisema kwenye video hiyo.

Kwenye video hiyo, Bi Wangari pia alifichua kuwa bosi wake Director Trevor na Mungai Eve hawajakuwa pamoja kwa takriban mwaka mmoja kwani walitengana Februari mwaka jana.

Pia alifichua kuwa Director Trevor alianza kufanya kazi ya mabadiliko ya kikazi alipotengana na mpenzi huyo wake wa muda mrefu mapema mwaka jana.

“Wawili hao waliamua kufanya kazi pamoja katika muda wa mwaka mmoja uliopita na sasa wameamua kwenda njia tofauti. Wawili hawa wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa mwaka mmoja lakini wametengana kwa mwaka mmoja,” alisema.

Mrembo huyo alieleza kuwa bosi wake na Mungai Eve hawakuwa wanakosea walipoonekana wakiwa na watu wengine mwaka jana kwani walikuwa wametengana.

Siku ya Jumatatu jioni, Director Trevor ambaye jina lake halisi ni Bonaventure Monyancha alitangaza mabadiliko kadhaa makubwa katika kampuni ya Mungai Eve Media ambayo yatatekelezwa Jumanne, Februari 20

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 alitangaza kuwa kampuni hiyo ya habari za mitandaoni itabadilisha jina lake kuwa Kenya Online Media.

"Je, uko tayari? Taarifa rasmi itashuka kesho," Director Trevor alitangaza.

Alifichua kuwa kutakuwa na mabadiliko kwenye chaneli za YouTube za Mungai Eve na Insta Fame zenye jumla ya wafuasi zaidi ya 850,000 pamoja na ukurasa wa Facebook wa Mungai Eve Media wenye takriban wafuasi 874,000

Wakati alipoulizwa ikiwa ataendelea kufanya kazi na mpenzi huyo wake wa muda mrefu, Trevor alisema kuwa huduma zake hazitahitajika tena.

"Hapana! Huduma zake hazihitajiki tena kwenye mifumo ifuatayo, YouTube – wanaofuatilia 754k, wanaofuatilia Insta Fame 104k, Facebook 874k," alisema.

Katika taarifa nyingine, mtaalam huyo wa mitandao ya kijamii alionekana kumrushia vijembe Mungai Eve akidokeza kuwa mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23 anafurahia matunda ya mti alioupanda muda mrefu uliopita.

"Kuna mtu ameketi kivulini leo kwa sababu mtu alipanda mti muda mrefu uliopita," aliandika.